Oct 30, 2021 03:23 UTC
  • Saudia yamwita nyumbani balozi wake wa Lebanon, yamtaka wa Lebanon pia aondoke nchini humo

Saudi Arabia imemwita nyumbani balozi wake wa Lebanon na kumtaka balozi wa nchi hiyo pia aondoke mjini Riyadh, likiwa ni jibu kwa matamshi ya ukosoaji aliyotoa waziri wa habari wa Lebanon kuhusiana na uchokozi na uvamizi wa kijeshi uliofanywa na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudia dhidi ya Yemen.

Serikali ya Saudia jana ilimwita nyumbani balozi wake wa mjini Beirut na kumpa balozi wa Lebanon mjini Riyadh muda wa masaa 48 awe ameshaondoka katika ardhi ya nchi hiyo.

Serikali ya Saudi Arabia imechukua uamuzi wa kusimamisha pia uingizaji nchini humo bidhaa zote zitokazo Lebanon.

Mivutano na mikwaruzano katika uhusiano wa Saudia na Lebanon imeshadidi kufuatia matamshi aliyotoa waziri wa habari wa Lebanon George Kordahi ya kulaani uchokozi na uvamizi dhidi ya Yemen uliofanywa na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudia. 

Akizungumza katika mahojiano aliyofanyiwa na chaneli moja ya televisheni na ambayo yalirekodiwa zaidi ya mwezi mmoja nyuma kabla ya kuteuliwa kuwa waziri na kurushwa hewani hivi karibuni, Kordahi alisema, uvamizi huo "hauna tija yoyote" na akasisitizia udharura wa kukomeshwa hujuma na mashambulio yanayofanywa na muungano wa kijeshi wa Saudia dhidi ya Yemen.

George Kordahi

Msimamo huo wa waziri wa habari wa Lebanon umeikasirisha sana Saudi Arabia na waitifaki wake katika Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi.

Mwezi Machi 2015 na kwa uungaji mkono wa Marekani, Imarati na nchi zingine kadhaa, Saudi iliivamia kijeshi Yemen na kuiwekea mzingiro wa ardhini, angani na baharini pia nchi hiyo masikini ya Kiarabu.

Moto wa vita uliowashwa na utawala wa Riyadh kwa ushirikiano na waitifaki wake dhidi ya Yemen, hadi sasa umeshateketeza roho za makumi ya maelfu ya watu, kuwajeruhi maelfu ya wengine na kuwafanya mamilioni kadhaa pia kuwa wakimbizi.

Umoja wa Mataifa ulitangaza hivi karibuni kuwa hali ya kibinadamu nchini Yemen ni ya maafa makubwa na ukasisitiza kwamba, nchi hiyo inakabiliwa na hali mbaya zaidi ya kibinadamu kuwahi kushuhudiwa duniani.../

Tags