Oct 30, 2021 07:45 UTC
  • Waziri Mkuu wa Lebanon asikitishwa na uamuzi wa Saudia kuhusiana na mabalozi wa nchi mbili

Waziri Mkuu wa Lebanon Najib Mikati amesema, amesikitishwa na uamuzi wa Saudi Arabia wa kumpa muhula maalumu balozi wa Lebanon awe ameshaondoka nchini humo sambamba na kumwita nyumbani balozi wake wa mjini Beirut.

Najib Mikati ametoa kauli hiyo kufuatia uamuzi uliochukuliwa na viongozi wa Riyadh kutokana na matamshi aliyotoa waziri wa habari wa Lebanon George Kordahi ya kulaani mashambulio ya muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya Yemen; na akasisitiza kuwa, kufanya juhudi za kuhuisha uhusiano wa kihistoria kati ya Lebanon na ndugu zake wa Kiarabu ni kipaumbele cha siku zote cha serikali ya Beirut.

Mbali na kuzitaka nchi za Kiarabu zifanye jitihada ili kudumisha mshikamano wa Waarabu na kuishinda migogoro iliyopo katika eneo, Mikati amesema, Lebanon nayo pia itaendelea kuwasiliana na pande zingine kwa ajili ya kushughulikia utatuzi wa migogoro ya eneo na athari zake hasi.

George Kordahi

Hayo yanajiri huku nchi zingine tatu wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi, ambazo ni Imarati, Bahrain na Kuwait, nazo pia zikichukua hatua ya kuwaita nyumbani mabalozi wao walioko Beirut.

Katika hatua ya karibuni kabisa, Bahrain imeungana na Saudia kwa kumtaka balozi wa Lebanon mjini Manama aondoke nchini humo.

Mbali na kumrejesha nyumbani balozi wake wa Beirut na kumpa balozi wa Lebanon masaa 48 hapo jana awe ameshaondoka katika ardhi ya Saudia, serikali ya Riyadh imesimamisha pia uingizaji wa bidhaa nchini humo zinazotoka Lebanon.../ 

Tags