Oct 31, 2021 02:21 UTC
  • Al Bukhaiti: Lengo la Saudia ni kuwapigisha magoti wananchi wa Lebanon

Mjumbe wa Baraza la Kisiasa la Harakati ya Ansarullah ya Yemen amesema kuwa hatua ya Saudi Arabia ya kumfukuza balozi wa Lebanon nchini humo ni kujaribu kuwapigisha magoti wananchi wa Lebanon na kuwafanya watumwa wake.

Muhammad al Bukhaiti amesema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na televisheni ya al Mayadeen na kuongeza kuwa, misimamo ya chuki inayochukuliwa na Saudia dhidi ya Lebanon ni kwa ajili ya kutumikia malengo ya mabeberu hasa Marekani na utawala wa Kizayuni na kuwashinikiza wananchi wa Lebanon ambao wamesimama imara kupambana na Wazayuni makatili.

Waziri wa Habari wa Lebanon, George Kurdahi Jumatatu iliyopita alisikika akisema katika programu iliyorekodiwa ya televisheni kwamba vita vilivyoanzishwa na Saudi Arabia huko Yemen havina maana na alilaani vita hivyo. Pia alisema, wananchi wa Yemen wana haki ya kujihami mbele ya madola yaliyoivamia nchi yao.

 

Ukweli huo mchungu umewaumiza sana watawala wa Saudi Arabia na ndio maana wamemfukuza balozi wa Lebanon nchini humo na kumwita nyumbani balozi wake kutoka nchini Lebanon.

Saudi Arabia imeamua pia kusimamisha biadhaa zake zote inazoziuza nchini Lebanon huku baadhi ya nchi za Kiarabu ikiwemo hata Kuwait nazo zikifuata mkumbo wa kulaani matamshi hayo yaliyotolewa zamani na Waziri wa Habari wa Lebanon licha ya kwamba ni kweli. 

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Lebanon Najib Mikati amesema, amesikitishwa na uamuzi wa Saudi Arabia wa kumpa muhula maalumu balozi wa Lebanon awe ameshaondoka nchini humo sambamba na kumwita nyumbani balozi wake wa mjini Beirut kutokana na matamshi hayo ya zamani ya Waziri wa Habari wa Lebanon, George Kurdahi.

Tags