Nov 01, 2021 03:08 UTC
  • Wanajeshi kadhaa wa Mali wauawa katika mashambulizi tofauti

Jeshi la Mali limetangaza habari ya kuuawa askari saba wa nchi hiyo katika mashambulizi mawili tofauti huko magharibi mwa nchi.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, msafara wa magari ya jeshi la Mali ulizingirwa na kushambuliwa na genge la wabeba silaha karibu na mji wa Mourdiah, yapata kilomita 200 kaskazini mwa Bamako, mji mkuu wa nchi hiyo, ambapo askari wawili waliuawa huku wengine watatu wakijeruhiwa.

Katika shambulio la pili lililojiri masaa mawili baada  ya hujuma ya kwanza, wanajeshi watano waliuawa baada ya gari lao kukanyaga bomu la kutegwa ardhini katika mji wa Segou, umbali wa kilomita 200 kaskazini mashariki mwa jiji la Bamako.

Jeshi la Mali pasi na kutaja genge lililohusika na hujuma hizo za Jumamosi limeeleza kuwa limewatia mbaroni watuhumiwa wawili wanaoshukiwa kuhusika na mashambulio hayo.

Magenge ya wabeba silaha Mali

Mapema mwezi uliopita wa Oktoba, wanajeshi 16 wa Mali waliuawa na wengine zaidi ya 11 kujeruhiwa kufuatia shambulio dhidi yao katikati mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika, lililofanywa na wapiganaji wenye mfungamano na makundi ya kigaidi ya al-Qaeda na ISIS (Daesh). 

Kwa mujibu wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Mali (MINUSMA), raia wasiopungua 527 wamekuwa waathirika wa moja kwa moja wa vurugu za ukiukaji wa haki za binadamu nchini Mali katika robo ya pili ya mwaka huu 2021, baadhi wakiwa wameuawa, kujeruhiwa, kutekwa nyara au kutoweka.

Tags