Nov 02, 2021 00:58 UTC
  • Sababu na malengo ya mashinikizo mazito ya Saudia na washirika wake dhidi ya Lebanon

Saudi Arabia imemwita nyumbani balozi wake mjini Beirut ikiwa ni jibu kwa matamshi yaliyotolewa na Waziri wa Habari wa Lebanon kuhusu vita vya Yemen. Riyadh pia imemfukuza balozi wa Lebanon nchini Saudi Arabia.

Nchi za Bahrain, Imarati na Kuwait pia zimefuata nyayo na kuwataka wanadiplomasia wa Lebanon kuondoka katika nchi hizo. 

Sababu ya hatua hiyo ya Saudia na nchi hizo tatu ndogo za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi dhidi ya Lebanon ni matamshi yaliyotolewa na Waziri wa Habari wa Lebanon, George Kurdahi, kuhusu vita vya Yemen. Yapata mwezi mmoja kabla ya kuteuliwa kwake kuwa waziri, Kurdahi alisema katika mahojiano yake na televisheni ya Aljazeera ya Qatar kwamba kuna udharura wa kusitisha mashambulizi dhidi ya watu wa Yemen na kuongeza kuwa, Saudi Arabia na nchi za Kiarabu za kandokando ya Ghuba ya Uajemi zinapaswa kukomesha vita hiyo isiyo na faida dhidi ya taifa la Yemen. Mahojiano hayo yalirushwa hewani Jumatatu iliyopita tarehe 26 Oktoba katika televisheni ya Aljazeera na kuibua msimamo mkali wa Saudia na nchi hizo tatu ndogo za Kiarabu. 

Swali linalojitokeza hapa ni kwamba, kwa nini matamshi ya George Kurdahi yamekabiliwa na msimamo huo mkali wa Saudia na washirika wake wa Kiarabu? Lengo la msimamo huo ni lipi? 

George Kurdahi

Inaonekana kuwa sababu kuu ya jibu na msimamo huo mkali ni hali ya sasa ya Aal Saud katika vita vyao huko Yemen. Watawala wa Saudia wanakabiliana na mashinikizo makubwa ya kikanda na kimataifa kutokana na vita hivyo ambavyo vimesababisha hali na mgogoro mkubwa zaidi wa binadamu katika karne ya 21. Kwa sasa Saudi Arabia na washirika wake wamekwama katika kinamasi cha Yemen huku wakiendelea kuandamwa na mashinikizo ya jamii ya kimataifa na fikra za walimwengu kutokana na jinai na uhalifu unaofanywa dhidi ya raia wasio na hatia wa Yemen. Hali imekuwa mbaya kiasi kwamba, hata serikali ya sasa ya Marekani imekosoa mara kadhaa vita vya Wasaudia huko Yemen.

Katika upande mwingine pia Saudi Arabia inashuhudia kusonga mbele na mafanikio ya jeshi na wapiganaji wa Ansarullah nchini Yemen hususan katika mkoa muhimu wa Ma'rib. Matamshi yaliyotolewa na Waziri wa Habari wa Lebanon, George Kurdahi pia yanawafanya walimwengu wamulike tena jinai zinazoendelea kufanywa na Saudia na washirika wake dhidi ya binadamu na kuweka wazi haki ya harakati ya Ansarullah ambayo inapigana kwa ajili ya kujihami na kulinda ardhi ya Yemen mbele ya hujuma na mashambulizi ya nchi vamizi. Kwa sababu hiyo yamewakasirisha sana Aal Saud na waitifaki wao.

Sababu nyingine inahusiana na mtazamo wa Saudi Arabia kuhusu yanayojiri nchini Lebanon. Saudia ni miongoni mwa nchi zinazoingilia masuala ya ndani ya Lebanon na zinazofanya jitihada za kutaka kuhakikisha kwamba, harakati ya Hizbullah haiwi na nafasi muhimu nchini humo. Baadhi ya wanasiasa wa Lebanon wanashirikiana na Riyadh katika kuibua fitina na migogoro nchini humo. Kiongozi wa kundi linalojiita The Lebanese Forces (LF), Samir Geagea ni miongoni mwa wanasiasa hao na ripoti zinasema amekutana na kufanya mazungumzo na balozi wa Saudia kabla ya kuondoka mjini Beirut. Samir Geagea ndiye aliyesimamia jinai iliyofanyika katika eneo la Tayune mjini Beirut tarehe 14 Oktoba ambapo waandamanaji 7 waliuawa kwa kupigwa risasi na wengine zaidi ya 60 kujeruhiwa. Hata hivyo msimamo imara wa Katibu Mkuu wa Hizbullah, Sayyid Hassan Nasrullah, na tahadhari yake kuhusu njama za kuzusha fitina ya ndani vimezima njama ya Tayune.

Wahanga wa jinai ya Tayune

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Nasim Berry anasema: "Hatua ya sasa ya Saudi Arabia haikuchukuliwa kujibu matamshi ya Waziri wa Habari wa Lebanon yaliyotolewa mwezi mmoja kabla ya kuundwa serikali ya Najib Mikati. Riyadh inatumia matamshi ya Kurdahi kama kisingizio cha kuhalalisha hatua zinazokusudia kuvunja mgongo wa Lebanon na kutoa dharba kubwa zaidi kwa nchi hiyo… Baada ya kufeli njama ya Tayune ya kuitumbukiza Lebanon katika fitina na vita vya ndani na kufuatia matamshi ya Kamanda wa Jeshi la Lebanon, Joseph Aoun aliyesisitiza kuwa Samir Geagea amehusika na jinai hiyo na kuitwa kwake mahakamani, Saudia imelazimika kutafuta njia ya kumuokoa kibaraka wake huyo nchini Lebanon. Kwa msingi huo matamshi ya Kurdahi ni kisingizio kinachotumiwa na serikali ya Riyadh kwa shabaha ya kuchochea fitina na mivutano nchini Lebanon.”    

Tags