Nov 02, 2021 12:23 UTC
  • Matamshi ya Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Saudi Arabia dhidi ya makundi ya muqawama Asia Magharibi

Faisal bin Farhan al-Saud, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Saudi Arabia amesema katika mahojiano na Kanali ya Televisheni ya al-Arabiya kwamba, matatizo na mvutano wa nchi yake na Lebanon ni zaidi ya matamshi ya waziri wa habari wa nchi hiyo, kwani Saudia haikubaliani kabisa na suala la kupata nguvu waitifaki wa Iran nchini Lebanon na katika eneo la Asia Magharibi kwa ujumla.

Faisal bin Farhan al-Saud  amesema hayo katika hali ambayo, ukosoaji uliorushwa hewani hivi karibuni wa Waziri wa Habari wa wa Lebanon George Kordahi kuhusiana na vita vya Yemen ambao aliutoa kabla ya kuwa waziri, umezua mgogoro baada ya Saudi Arabia kukasirishwa na matamshi hayo na kuchukua hatua ya pupa ya kumuita nyumbani balozi wake kutoka Beirut na kumfukuza balozi wa Lebanon mjini Riyadh, huku nchi nyingine kama Bahrain, Imarat na Kuwait nazo zimefuata mkumbo huo.

Matamshi ya Faisal bin Farhan yanaonyesha kuwa, Saudia imekasirishwa mno na mwenendo wa matukio ya Asia Magharibi na kubadilika nguvu ya mlingano kwa maslahi ya mhimili wa muqawama kwa uongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Utawala wa Aal Saud unaihesabu Hizbullah ya Lebanon kama muitifaki na mshirika muhimu kabisa wa Iran katika eneo la Asia Magharibi, na hivi sasa ukitumia kisingizio cha matamshi ya Kordahi kwa mara nyinyine tena unafanya juhudi za kuishinikiza Hizbullah ya Lebanon.

Wanamapambano wa Hizbullah ya Lebanon

 

Kuhusiana na hilo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Saudi Arabia ametangaza kinagaubaga kwamba, Lebanon inahitajia mageuzi jumla na sababu ya hitajio la mageuzi hayo ni satwa na nguvu ya Hizbullah katika maamuzi ya kimsingi na muhimu ya nchi hiyo. Aidha Faisal bin Farhan al Saud ameongeza kuwa, suala la Hizbullah kuwa na satwa na mamlaka katika mfumo wa kisiasa wa Lebanon ni jambo ambalo linatutia  wasiwasi na kulifanya suala la ushirikiano wa Lebanon na Saudia kutokuwa na faida.

Katika kipindi cha muongo mmoja wa hivi karibuni Saudi Arabia imetumia njia mbalimbali kuhakikisha kuwa, inaudhoofisha muqawama na baada ya kufeli katika njama zake hizo, hivi sasa inahaha kuhakikkisha kuwa, inazuia kuimarika zaidi mhimili wa muqawama na kubadilisha pia mlingano wa nguvu katika eneo la Asia Magharibi. Hata hivyo, katika hili pia Saudi Arabia imegonga mwamba. Dola za pato la mafuta ya Saudia zimeingia katika mifuko ya madola makubwa ya Magharibi hususan Marekani, lakini kinyume na matarajio  ya watawala wa ukoo wa al Saud, nafasi ushawishi wa Riyadh katika eneo badala ya kupata nguvu unazidi kudhoofika siku baada ya siku.

 

Utawala wa Saudia unaamini kuwa, uongozi wa Iran kwa mhimili wa muqawama na utiifu wa makundi ya muqawama kwa Jamhuri ya Kiislamu ndio chimbuko  la kushindwa kwake kufikia malengo yake.  Kwa muktadha huo, katika hali ambayo, yenyewe Saudia haina hata demokrasia ya kiwango cha chini tu, imekuwa ikitumia gharama kubwa kwa ajili ya kutoa pigo dhidi ya waitifaki wa Iran nchini Lebanon na Iraq.

Matamshi ya Faisal bin Farhan al-Saud, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Saudi Arabia yanaonyesha wazi kuwa, Riyadh inayatumia matamshi ya ukosoaji wa George Kordahi kuhusu vita vya Saudia huko Yemen  kama kisingizio cha kuleta vurugu na ukosefu mwingine wa amani nchini Lebanon, ili kwa njia hiyo iweze kufikia malengo yake yaliyo dhidi ya muqawama.

Saudi Arabia imefanya mauaji mengi na jinai za kkutisha kkatika vita vyake dhidi ya Yemen

 

Nukta yenye umuhimu mkubwa ni hii kwamba, Saudia imeanzisha duru mpya ya mashinikizo dhidi ya Lebanon katika hali ambayo, Mwezi Machi mwaka ujao wa 2022 Lebanon inatarajiwa kufanya uchaguzi wa Bunge. Kwa maneno mengine ni kuwa, imebakia takribani miezi minne kabla ya kufanyika uchaguzi wa Bunge nchini Lebanon.

Saudi Arabia na waitifaki wake katika Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi wanaishinikiza Lebanon ili kwanza waandae mazingira ya kuvuruga muungano wa muqawama katika uchaguzi ujao, na endapo watafikia natija hii kwamba, hakuna uwezekano wa kuushinda muqawama, basi watekeleza mpango wa pili ambao ni kuzusha machafuko na vurugu za barabnarani, na hivyo kuandaa mazingira ya kuakhirishwa uchaguzi wa Bunge nchini Lebanon.

Tags