Nov 03, 2021 02:28 UTC
  • Hamaki za Israel hata kwa “ripoti isiyo na dhamana” ya Baraza la Haki za Binadamu la Umioja wa Mataifa

Kitendo cha mwakilishi wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Gilad Erdan cha kurarua na kuchanachana kwa hasira ripoti ya Baraza la Haki za Binadamu la umoja huo kuhusu jinai za utawala huo huko Palestina kimeonyesha wazi kwamba, utawala huo hauwezi kuvumilia hata ripoti ambazo kimsingi “hazina dhama ya utekelezwaji wake”.

Akihutubia Oktoba 29 ya mwezi uliopita katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa huku akiwa amehamaki, Gilad Erdan mbali na kuchana ripoti ya Baraza la Haki za Binadamu iliyokuwa ikieleza jinai za Israel alisema kwa ujeuri kwamba, mahala pa ripoti hiyo ni jalalani. Kitendo hiki cha kishenzi cha mwakilishi huyo wa Israel katika Umoja wa Mataifa kinaweza kutathminiwa na kuchunguzwa katika pande kadhaa.

Upande wa kwanza, unahusiana na hasira ya Israel ya kufichuliwa kwa kiwango kikubwa ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na utawala huo ghasibu.

Ripoti yake hiyo ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa imeelezea mambo mengi yaliyo kinyume cha sheria yanayofanywa na Wazayuni, kwa kuashiria jinai zinazofanywa na Israel huko Palestina, ujenzi wa vitongoji haramu vya walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina, hali ya haki za binadamu katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na miinuko ya Golan na haki ya Wapalestina ya kujiainishia hatima na mustakabali wao.

Kila moja kati ya yaliyotajwa ni jinai ambazo zimekuwa zikifanywa kwa sura ya mwenendelezo na tena kila uchao na utawala ghasibu wa Israel dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina. Pamoja na unyama wote huo, viongozi wa Israel wasio na utu wala ubinadamu wanataraji kwamba, kusitolewa ripoti kama hizi dhidi ya Israel hasa kutokana na lobi zenye nguvu zilizoko ndani ya madola ya Magharibi hususan Marekani.

Watoto wa Kipalestina wahanga wakuu wa jinai na ukandamizaji wa utawala haramu wa Kiizayuni wa Israe

 

Upande wa pili, unahusiana na utendaji wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kuhusiana na faili la Israel kuhusiana na haki za binadamu. Baraza hilo lina utaratibu unaojulikana kama The Universal Periodic Review (UPR) ambao ni kufanya mapitio jumla ya kila kipindi fulani kuhusu kuheshimiwa suala la haki za binadamu na wanachama wa baraza hilo.

Kama alivyokiri Gilad Erdan ni kuwa, tangu Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa liasisiwe miaka 15 iliyopita, katika kipindi chote hiki kumetolewa maazimio 95 dhidi ya Israel peke yake huku kukitolewa maazimio 142 tu dhidi ya mataifa mengine duniani. Kwa maneno mengine ni kuwa, katika kipindi cha miaka 15 iliyopita, Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa limepasisha jumla ya maazimio 237 huku 95 yakiwa ni dhidi ya Israel. Takwimu hizi zinaweka wazi jinsi Israel inavyokiuka na kukanyaga kwa wigo mpana haki za binadamu hususan dhidi ya Wapalestina.

Upande wa tatu, unahusiana na kitendo  chenyewe cha mwakilishi wa Israel cha kurarua hadharani ripoti ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa. Hatua hiyo inathibitisha wazi kuwa, utawala vamizi wa Israel hauziheshimu katu asasi za jumuiya za kimataifa hususan Umoja wa Mataifa na asasi zinazofanya kazi chini yake.

Maandamano ya kususia bidhaa za Israel

Desemba 2016 Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio 2334 ambalo liliutaka utawala haramu wa Israel usimamishe haraka na kikamilifu shughuli zote za ujenzi wa vitongoji katika ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu. Baada ya azimio hilo, siyo tu kwamba, Israel imesimamisha ujenzi wa vitongoji hivyo vya walowezi wa Kizayuni, bali imeongeza kasi ya ujenzi wake ambapo ni hivi majuzi tu ambapo ilipasisha mpango wa kujengwa nyumba mpya zaidi ya 3,000 katika ardhi unazozikalia kwa mabavu.

Weledi wa mambo wanaamini kuwa, kile ambacho kinaupa kiburi utawala huo cha kuendelea kukiuka haki za binadamu na kupuuza maazimio ya Umoja wa Mataifa ni himaya na uungaji mkono au kimya cha madola makubwa ya Magharibi kuhusiana na hatua na jinai za Israel katika uga wa haki za binadamu.

Ni kwa kuzingatia ukweli huo, ndio maana Kazem Gharib Abadi, Katibu wa Tume ya Haki za Binadamu ya Mhimili wa Mahakama wa Iran amesema kuwa, kimya cha wanaoitwa waungaji mkono wa haki za binadamu ndio sababu ya ufidhuli na ujeuri uliofanywa na utawala bandia wa Israel katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Gharib Abadi ameeleza hayo katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter na kueleza bayana kwamba: Kimya cha mataifa yanayojulikana kama eti watetezi wa haki za binadamu kwa ukiukaji wa kutisha na wa mara kwa mara wa haki za binadamu unaofanywa na utawala wa Kizayuni ndio ulioupa uthubutu utawala huo wa kuichanachana ripoti ya Mwenyekiti wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa na kulidhihaki baraza hilo.

Vitongoji vya walowezi wa Kizayuni

 

Upande wa nne ni kuwa, kama Umoja wa Mataifa utashindwa kukabiliana na vitendo kama hivi na kutetea uwepo na heshima yake, basi kivitendo utakuwa unajitusi wenyewe na mwisho wa siku ni kutokuwa na hadhi na itibari yoyote mbele ya walimwengu na wapenda haki duniani. Hata hivyo kwa kuzingatia kuwa, madola Magharibi na hasa Marekani yana ushawishi mkubwa ndani ya Umoja wa Mataifa, haitarajiwi kama umoja huo japo utajitutumua na kutetea heshima na hadhi yake mbele ya wanaoudhihaki na kuucheza shere.

Ripoti na maazimio ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kuhusiana na ukiukaji wa haki za binadamu wa Israel kimsingi hayana dhamana ya kutekelezwa bali yanaweza kuhesabiwa kuwa lengo ni kutoa nasaha tu. Lakini pamoja na hayo, hata nasaha zinaonekana kuwakera na kuwakasirisha viongozi wa utawala haramu wa Israel.

Tags