Nov 03, 2021 12:37 UTC
  • Sheikh Hassan al Baghdadi
    Sheikh Hassan al Baghdadi

Mjumbe wa Baraza Kuu la la chama cha Hizbullah nchini Lebanon amesema kuwa nchi hiyo haitasalimu amrii mbele ya mashinikizo na vitisho vya Saudi Arabia.

Sheikh Hassan al Baghdadi ameyasema hayo kufuatia mgogoro ulioibuka baina ya Lebanon na Saudi Arabia na kuongeza kuwa, miongoni mwa matatizo ya kimsingi ya Saudia na utawala wa Kizayuni wa Israel ni kwamba hazijifunzi na kuchukua ibra kutokana na hatua zao za huko nyuma.

Al Baghdadi amesema kuwa, Saudi na Israel hazitaki kujifunza kutokana na yaliyopita na kuongeza kuwa, viongozi wa tawala hizo maghasibu wanapaswa kuelewa kuwa, Lebanon haitasalimu amri kwa mashinikizo na vistisho. 

Saudi Arabia imemwita nyumbani balozi wake mjini Beirut na kumfukuza balozi wa Lebanon mjini Riyadh kufuatia matamshi yaliyotolewa na Waziri wa Habari wa Lebanon, George Kurdahi kuhusu vita vya Yemen. Yapata mwezi mmoja kabla ya kuteuliwa kwake kuwa waziri, Kurdahi alisema katika mahojiano yake na televisheni ya Aljazeera ya Qatar kwamba kuna udharura wa kusitisha mashambulizi dhidi ya watu wa Yemen na kuongeza kuwa, Saudi Arabia na nchi za Kiarabu za kandokando ya Ghuba ya Uajemi zinapaswa kukomesha vita hiyo isiyo na faida dhidi ya taifa la Yemen. 

Nchi za Bahrain, Imarati na Kuwait pia zimefuata nyao na kuwarejesha nyumbani wanadiplomasia waliokuwa nchini Lebanon. 

Tags