Nov 04, 2021 12:02 UTC
  • Israel: Hizbullah ina uwezo wa kutupiga kwa maelfu ya makombora kila siku

Kamanda wa Operesheni za Kambi ya Ndani ya utawala wa Kizayuni wa Israel amekiri kuwa, harakati ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon ina uwezo mkubwa wa makombora ambao unaiwezesha kuushambulia utawala wa Kizayuni kwa maelfu ya makombora kila siku kama vita baina ya pande hizo mbili vitatokea.

Televisheni ya al Mayadeen imemnukuu Auri Gordin, Kamanda wa Operesheni za Kambi ya Ndani ya utawala wa Kizayuni wa Israel akikiri hayo leo Alkhamisi na kuongeza kuwa, iwapo vita vitatokea, basi Hizbullah ina uwezo wa kuishambulia Israel kwa maelfu ya makombora kila siku.

Nalo gazeti la Kizayuni la Maariv limeandika katika ripoti yake kuwa, jeshi la Israel limechora hali kadhaa zinazoweza kutokea iwapo utawala huo utaingia katika vita na Hizbullah ya Lebanon na muhimu zaidi ni uwezekano wa Hizbullah kushambulia maghala yenye mada hatari za kemikali katika mji wa Haifa na kuisambaratisha bandari ya mji huo wa Haifa kwa makombora yake yenye ustadi mkubwa wa kupiga shabaha.

Meja Jenerali Auri Gordin, Kamanda wa Operesheni za Kambi ya Ndani ya utawala wa Kizayuni wa Israel

 

Nayo kanali ya 13 ya televisheni ya utawala wa Kizayuni wa Israel imesema katika ripoti yake kwamba makundi ya muqawama ya Hizbullah kutokea kaskazini mwa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni au Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS kutokea kusini mwa ardhi hizo, yanaweza kutumia droni na ndege zisizo na rubani zinazojiripua zenyewe, kushambulia maeneo nyeti na muhimu sana ya Israel.

Mara kwa mara majenerali wa ngazi za juu wa jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel wamekuwa wakitahadharisha kuhusu uwezekano wa kushambuliwa vibaya sana Israel kwa makumi ya maelfu ya makombora ya Hizbullah iwapo vita vitatokea.

Tags