Nov 06, 2021 03:25 UTC
  • Hizbullah yaitaka Saudia iiombe radhi Lebanon

Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesema Saudi Arabia inapaswa kuliomba radhi taifa la Lebanon kutokana na mienendo yake ya kiuhasama dhidi ya wananchi wa nchi hiyo ya Kiarabu.

Sheikh Naeem Qassim amesema hayo katika mahojiano na kanali ya televisheni ya al-Manar na kusisitiza kuwa, "Saudia imeanzisha vita dhidi ya Lebanon."

Amebainisha kuwa, Riyadh inapaswa kuwaomba radhi wanachi wa Lebanon kutokana na vitendo vyake ghalati na vya kiuadui, na ambavyo vinakiuka misingi yote ya maadili.

Kiongozi huyo wa kidini nchini Lebanon ameeleza kuwa, hatua za kiuhasama zilizochukuliwa hivi karibuni na Saudia dhidi ya Lebanon zimetokana na hamaki za Aal-Saud kushindwa kudhibiti maamuzi muhimu ya kisiasa ya Lebanon, licha ya kumwaga fedha nyingi kwa waungaji mkono wake.

Waziri wa Habari wa Lebanon aliyelaani vita vya muungano vamizi wa Saudia dhidi ya Wayemen

Kadhalika Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesema hatua hizo za Saudi Arabia zinalenga kupotosha fikra za waliowengi, kutokana na kushindwa kwake vibaya katika vita vyake dhidi ya Yemen.

Hivi karibuni, Riyadh ilitangaza kukata uhusiano wake wa kidiplomasia na Beirut, kufuatia matamshi yaliyotolewa na Waziri wa Habari wa Lebanon, George Kurdahi kuhusu vita vya Yemen. Kama ilivyotarajiwa, Bahrain, Imarati na Kuwait zilifuata kibubusa mkumbo huo wa Saudia, na kuwarejesha nyumbani mabalozi wao waliokuwa nchini Lebanon. 

Tags