Nov 07, 2021 03:41 UTC
  • Jihad al Islami yatoa onyo kali kwa utawala wa Kizayuni wa Israel

Kiongozi mmoja mwandamizi wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Jihad al Islami wa Palestina ametoa onyo kali kwa utawala wa Kizayuni wa Israel akitahadharisha kuwa, kama mateka mmoja tu wa Palestina atauawa shahidi, basi utawala huo utalipa jinai yake hiyo.

Kwa mujibu wa televisheni ya al Mayadeen, Khaled al Batsh alitoa onyo hilo jana Jumamosi mbele ya mjumuiko wa Wapalestina waliokusanyika mbele ya ofisi ya Msalaba Mwekundu huko Ghaza Palestina ili kutangaza mshikamano wao na mateka wa Kipalestina walioko mikononi mwa utawala katili wa Israel.

Amesema, adui Mzayuni anapaswa kutambua kuwa, harakati ya Jihad al Islami kamwe haitowaacha peke yao mateka wa Palestina wanaogoma kula chakula na itafanya juhudi zake zote kuhakikisha wanaachiliwa huru.

Jela ya Gilboa ya Israel yenye ulinzi mkali

 

Vile vile amewataka wapatanishi kuchukua hatua za haraka za kuwaokoa mateka wa Palestina wanaondesha mgomo wa kula na vile vile waulazimishe utawala wa Kizayuni ukomeshe vitendo vyake vya dhulma dhidi ya mateka wa Kipalestina kwenye jela za kuogofya za Wazayuni.

Utawala wa Kizayuni wa Israel umeongeza sana jinai zake dhidi ya mateka wa Palestina hasa baada ya mateka sita kufanikiwa kutoroka kishujaa katika jela yenye ulinzi mkali ya Gilboa ya utawala wa Kizayuni. Kufanikiwa kutoroka mateka hao lilikuwa pigo kubwa kwa muundo na mfumo wa kiusalama wa Israel ambao haukutarajia kabisa kuwa mateka wa Palesitna wanaweza kufanya kitendo cha kishujaa kama hicho.

Baadhi ya mateka wa Kipalestina wanaoshikiliwa kwenye jela za kutisha za Israel wameamua kuendesha mgomo wa kutokula chakula ili kulalamikia jinai wanazofanyiwa na utawala huo katili.

Tags