Nov 14, 2021 11:12 UTC
  • Kufichuliwa jinai za kivita za jeshi la Marekani nchini Syria

Gazeti la New York Times limetoa ripoti inayoonyesha kuwa, jeshi la Marekani limetenda uhalifu wa kivita kwa kuua makumi ya wanawake na watoto katika mashambulio ya anga liliyofanya nchini Syria kwa kisingizio cha kile kinachoitwa mapambano dhidi ya kundi la DAESH (ISIS).

Jeshi la Marekani limeficha taarifa za mashambulio ya anga liliyofanya nchini Syria mwaka 2019 yaliyoua zaidi ya wanawake na watoto 64.

Mnamo tarehe 18 Machi 2019, kikosi cha anga cha jeshi la Marekani kilifanya mashambulio mawili mtawalia ya anga  karibu na mji wa Baghuz. Mashambulio hayo yalifanywa kwa amri ya kituo cha Marekani cha operesheni maalumu za kijeshi ambacho kilikuwa na jukumu la kuongoza operesheni za mashambulio ya nchi kavu nchini Syria.

Wakili mmoja wa kikosi cha anga cha Marekani, ambaye wakati huo alikuwemo kwenye kituo hicho cha operesheni maalumu, alisema, kulikuwa na uwezekano wa mashambulio hayo kuwa ni jinai za kivita; na baadaye akatoa indhari hiyo kwa mkaguzi mkuu wa wizara ya ulinzi, Pentagon na kamati ya vikosi vya ulinzi ya Seneti ya Marekani, lakini haikuchukuliwa hatua yoyote kuhusiana na indhari aliyotoa.

Mkaguzi mkuu wa Pentagon alianzisha uchunguzi kuhusu tukio la Machi 18, lakini katika ripoti aliyotoa, hakuashiria chochote kuhusu mashambulio hayo ya anga na wala haukuwahi tena kufanywa uchunguzi huru na kamili juu ya kadhia hiyo. Na mwisho wa wote, jeshi la Marekani pia likaamua kujisahaulisha na kulipuuza suala hilo.

Hivi sasa, na baada ya kutolewa ripoti ya gazeti la New York Times iliyofichua taarifa mpya kuhusu vitendo vya kihalifu vilivyofanywa na jeshi la Marekani nchini Syria, yameabainika yale ambayo hayakuwekwa wazi hapo kabla kuhusu kile kiitwacho operesheni za kupambana na Daesh zinazotekelezwa na Marekani nchini humo.

Muungano wa kimataifa wa kijeshi wa kupambana na DAESH (ISIS) ambao unaongozwa na Marekani, uliasisiwa mwaka 2014 na kuanza operesheni zake nchini Syria kwa kisingizio cha kukabiliana na kundi hilo la ukufurishaji. Ukweli ni kwamba, muungano huo wa kijeshi umefanya mashambulio mengi dhidi ya raia wa Syria na kupelekea kuuawa na kujeruhiwa idadi kubwa ya watu wasio na hatia. Umoja wa Mataifa umeeleza katika ripoti zake kadhaa kwamba, mashambulio yanayofanywa nchini Syria na muungano wa kimataifa unaoongozwa na Marekani kwa lengo la eti kupambana na DAESH yana hali inayolingana na uhalifu wa kivita.

Kwa kutegemea maoni na mitazamo ya wataalamu wa sheria za kimataifa, Ghassan Ramadhan Yousuf, mwandishi raia wa Syria, ameashiria jinai za kivita zilizofanywa na Marekani nchini humo na kueleza kwamba: Hatua za Marekani nchini Syria ni uhalifu wa kivita na uko kwenye kiwango cha jinai dhidi ya binadamu.

Suali linaloulizwa sasa ni kwamba, ikiwa mauaji ya raia yaliyofanywa katika operesheni ya mashambulio ya anga ni jinai ya kivita, kwa nini Marekani si tu haitoi maelezo ya kukubalika kuhusu sababu za kuwaua raia wa Syria katika mashambulio kadhaa iliyofanya, lakini kimsingi hasa imekuwa ikilipuuza suala hili na hata kulichukulia kuwa ni aina ya maafa yasiyoweza kuepukika?

Uchunguzi na uhakiki uliofanywa kuhusiana na nyaraka na ushahidi uliopo unaonyesha kuwa, katika mashambulio ya anga ziliyofanya nchini Syria, mara nyingi ndege za kivita za Marekani zimefanya dharau kwa kutochukua tahadhari ya kutosha kuhakikisha kiwango cha maafa ya raia kinakuwa ni cha chini kabisa. Ukweli ni kwamba, mengi ya mashambulio hayo ya anga yalikuwa makubwa kupita kiasi na yasiyo na mlingano au yalifanywa bila ya lengo lolote.

Ndege za kivita za Marekani zikifanya mashambulio ya anga Syria

Inavyoonyesha, kama kuna kitu kisicho na umuhimu kwa Washington na washirika wake, basi ni roho za watu wasio na hatia wanaouliwa na kujeruhiwa katika mashambulio hayo ya anga. Na hicho ni kielelezo na mfano wa wazi kabisa wa jinai za kivita.

Serikali ya Syria imechukua hatua mara kadhaa kuutaka Umoja wa Mataifa na baraza lake la usalama zikomeshe jinai zinazofanywa na Marekani nchini humo. Kimsingi hasa ni kwamba, uingiliaji kijeshi wa Marekani na waitifaki wake nchini Syria kupitia kile kinachoitwa muungano wa kimataifa wa kupambana na Daesh (ISIS), haujawa na matokeo mengine ghairi ya kuua raia na kuwaongezea mateso na machungu watu wa nchi hyo.

Ripoti ya karibuni ya gazeti la New York Times, nayo pia imetilia mkazo tena ukweli kuhusu hatua zisizo za kiutu na jinai za kivita zinazofanywa na jeshi la Marekani nchini Syria, huku ikiendelea kuyakalia kwa mabavu na kinyume cha sheria baadhi ya maeneo ya ardhi ya nchi hiyo.../

Tags