Nov 15, 2021 11:43 UTC
  • Hizbullah: Saudia inataka kuudhoofisha muqawama Lebanon

Afisa mwandamizi wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema lengo kuu la Saudi Arabia kuibua mzozo wa kidiplomasia baina ya Lebanon na nchi za Ghuba ya Uajemi ni kudhoofisha mrengo wa muqawama na kulipigisha magoti taifa hilo la Kiarabu.

Sheikh Ali Da’moush, Naibu Rais wa Baraza Kuu la Hizbullah ya Lebanon ameeleza bayana kuwa, "Hatutaki mgogoro hata kidogo, ama na Saudi Arabia au nchi nyingine yoyote ya Ghuba ya Uajemi. Tunatumai uhusiano wa Lebanon na ndugu zetu Waarabu utabaki imara, lakini si kwa gharama ya (kupoteza) mamlaka yetu ya kujitawala na heshima."

Sheikh Da'moush amesisitiza kuwa, wabunge wa Kongresi na maafisa wengine wa Marekani wamekuwa wakiukosoa muungano wa kijeshi wa Saudia dhidi ya Yemen sambamba na mzigiro wa kila upande dhidi ya taifa hilo maskini la Kiarabu, lakini Riyadh haithubutu kujibu na kutoa radiamali.

Afisa huyo wa ngazi ya juu wa Hizbullah ya Lebanon ameongeza kuwa, lengo haswa la hatua zinazochukuliwa na Saudia ni kuiwekea kizingiti kambi ya muqawama inayopambana na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Walebanon wakipeperusha bendera ya nchi yao na ya Hizbullah

Hata hivyo amesisitiza kuwa, kampeni za namna hiyo za kujaribu kuudhoofisha mrengo wa muqawama nchini Lebanon daima zimekuwa zikigonga mwamba. 

Hivi karibuni, Riyadh ilitangaza kukata uhusiano wake wa kidiplomasia na Beirut, kufuatia matamshi yaliyotolewa na Waziri wa Habari wa Lebanon, George Kurdahi kuhusu vita vya muungano wa Saudia dhidi ya Yemen. Nchi kadhaa waitifaki wa Saudia zimefuata mkumbo huo. 

Tags