Nov 17, 2021 13:39 UTC
  • Wanajeshi wa Israel wavamia Quds na mabuldoza yao na kuharibu mali za Wapalestina

Mabuldoza ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel yamevamia maeneo ya kaskazini mwa mji wa Quds na kuharibu mali na miliki za Wapalestina katika maeneo hayo.

Ripoti zaidi kutoka Quds zinasema kuwa, wanajeshi wa Israel wakiongozwa na mabuldoza wamevamia kitongoji kimoja jirani na kivuko cha Qalandiya kaskazini mwa Quds inayokaliwa kwa mabavu na kuharibu mali na miliki kadhaa za Wapalestina.

Wanajeshi hao wasio na huruma wa Israel wamevamia maduka, nyumba na vyanzo kadhaa vya kudhamini maisha vya Wapalestina na kuviharibu kabisa.

Mmoja wa Wapalestina aliyeharibiwa milki yake amenukuliwa na duru za habari akisema: Ardhi hii ni mali ya Wapalestina, hivyo hakuna mtu yeyote mwenye haki ya kutumia kisingizio cha sisi kutokuwa na kibali na kuharibu mali zetu. Kimsingi Wazayuni hawawapatii Wapalestina kibaki cha aina yoyote ile.

Wakati huo huo, Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) imesema katika ripoti yake kwamba, vitendo vya ukandamizaji vinavyofanywa na Israel vimeshadidi mno tangu kuanza mwaka huu wa 2021.

Buldoza la Israel likibomoa moja ya nyumba ya ghorofa ya Wapalestina

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, mwaka uliopita wa 2020 utawala wa Kizayuni wa Israel ulibomoa nyumba karibu 689 katika Ukingo wa Magharibi na Quds tukufu na kulazimisha mamia ya familia za Wapalestina kuwa wakimbizi.  

Utawala huo haramu umeendelea kubomoa nyumba na makazi ya Wapalestina licha ya Baraza ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutoa azimio nambari 2334 tarehe 23 Disemba mwaka 2016 ambalo liliutaka utawala huo kukomesha mara moja shughuli zote za ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi zote za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.   

Tags