Nov 19, 2021 11:47 UTC
  • George Kordahi: Hizbullah ndio tatizo hasa kwa Saudia katika uhusiano wake na Lebanon

Waziri wa Habari wa Lebanon amesema, tatizo hasa la Saudi Arabia na nchi yake halitokani na matamshi aliyotoa yeye hivi karibuni, bali linahusiana na harakati ya muqawama ya nchi hiyo, Hizbullah.

George Kordahi amesema leo kuwa, yeye anakaribisha njia yoyote ya utatuzi kwa ajili ya manufaa na maslahi ya kitaifa ya Lebanon na akaongeza kuwa, yuko tayari kujiuzulu wadhifa wake kwa ajili ya kufungua njia ya uhusiano wa Lebanon na nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi.

Kordahi amefafanua kwa kusema, "watu wote wanajua, tatizo lililopo hivi sasa katika uhusiano wa Riyadh na Beirut ni kubwa zaidi kuliko linavyohusishwa na mimi; na linahusu msimamo wa Saudi Arabia mkabala na nafasi ya Hizbullah ndani ya Lebanon na katika eneo, jambo ambalo Riyadh yenyewe imeshalieleza kinagaubaga mara kadhaa."

George Kordahi

Waziri wa Habari wa Lebanon vilevile amezungumzia sababu ya kutofanyika vikao vya Baraza la Mawaziri la nchi hiyo na akasema, "sababu ya kwanza inayokwamisha kufanyika kikao cha baraza la mawaziri ni tofauti zilizopo kuhusu Jaji Tariq Bitar, mkaguzi wa faili la mripuko wa bandari ya Beirut; lakini mbali na hilo, kwa kuwemo au kutokuwemo mimi, serikali inakabiliwa na changamoto kubwa sana za matatizo ya kimaisha, kijamii, kiuchumi na kifedha."

Mivutano ya karibuni baina ya Lebanon na nchi za Ghuba ya Uajemi na hasa Saudi Arabia, ilianza baada ya waziri wa habari wa Lebanon George Kordahi kutoa wito wa kukomeshwa vita vilivyoanzishwa na muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudia dhidi ya Yemen.

Kordahi alitoa wito huo katika mahojiano na televisheni ya Aljazeera ya Qatar aliyofanyiwa huko nyuma kabla ya kuteuliwa kuwa waziri wa habari katika serikali ya sasa ya Lebanaon.

Kufuatia kurushwa hewani mahojiano hayo, Saudia, Bahrain, Imarati na Kuwait ziliamua kuwarejesha nyumbani mabalozi wao waliokuwako Beirut, huku Saudi Arabia ikienda mbali zaidi kwa kuchukua uamuzi wa kusimamisha kuingizwa nchini humo bidhaa zinazotoka Lebanon.../ 

Tags