Nov 20, 2021 04:45 UTC
  • Safari za kidiplomasia nchini Syria; kushindwa siasa za kuitenga

Kufanyika safari za kidiplomasia nchini Syria ni dalili ya wazi kwamba siasa za wapinzani za kujaribu kuitenga serikali ya Damascus zimegonga mwamba.

Karibuni hivi, Alexander Lavrentyev, Mjumbe Maalumu wa Rais wa Russia katika Masuala ya Syria alifanya safari nchini humo ambapo alikutana na kuzungumza na viongozi wa ngazi za juu wa serikali ya Damascus. Katika mazungumzo hayo mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu alisema juhudi za kubuni serikali kivuli na isiyochaguliwa na Wasyria wenywe ni jambo lisilokubalika kabisa. Amesisitiza kwamba serikali ya nchi hiyo inapasa kuheshimiwa na mashambulio ya mara kwa mara ya utawala haramu wa Israel pia yasimamishwe.

Kabla ya hapo Abdallah bin Zayed, Waziri wa Mambo ya Nje wa Imarati na baada ya kupita miaka kumi, alielekea Syria ambako alikutana na kuzungumza na Rais Bashar al- Asad wa nchi hiyo. Safari hizo za kidiplomasia kwa upande mmoja zinaonyesha kuwa siasa za kujaribu kuitenga Syria zimegonga ukuta na kwa upande wa pili zinathibitisha kwamba nchi za Kiarabu zimeamua kuhuisha uhusiano wao na serikali ya Damascus.

Alexander Lavrentyev

Katika muongo mmoja uliopita, pande nne za nchi za Kiarabu, Magharibi,utawala wa Kizayuni na Uturuki zimetumia magaidi kutoa mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa dhidi ya serikali ya Bashar al-Asad kwa lengo la kuiangusha serikali yake na kubadilisha muundo wa utawala wa Syria kwa kuwaweka madarakani watawala vibaraka. Hata kama lengo la mashinikizo hayo limedaiwa kuwa ni kuleta demokrasia katika nchi hiyo ya Kiarabu lakini ni wazi kuwa siasa hizo zimekuwa zikifuatiliwa kwa ajili ya kuitenganisha Syria na mrengo wa mapambano.

Katika kukabiliana na mashinikizo hayo, Syria nayo iliamua kuunga mkono mrengo wa mapambano kwa nguvu zake zote, ambapo matokeo yake yamekuwa ni kuhifadhiwa ardhi yote ya nchi hiyo, kuendelea kusalia madarakani Bashar al-Asad na kuimarishwa mrengo wa mapambano Asia Magharibi (Mashariki ya Kati). Hakika ushindi wa Syria katika kukabiliana na magaidi na waungaji mkono wao na vilevile safari za kidiplomasia za karibuni ni matokeo ya moja kwa moja ya kusimama imara katika medani ya mapambano.

Mbali na Imarati, utawala haramu wa Israel na Marekani ni wachezaji wengine ambao wamekubali kushindwa katika siasa zao za kujaribu kuitenga Syria. Mashambulio yanayofanywa mara kwa mara na utawala huo haramu katika ardhi ya Syria, kabla ya jambo lolote lile ni dalili ya wazi kwamba utawala huo umekata tamaa kuhusiana na suala zima la kuondolewa madarakani serikali ya hivi sasa ya Syria.

Gazeti la ar-Rai al-Yaum limeandika karibuni kwamba: Baada ya kutolewa ripoti nyingi kuhusu hatua ya baadhi ya nchi za Kiarabu kuimarisha uhusiano wao na Damascus, hatua ambayo wajuzi wa mambo wanasema imechukuliwa kufuatia alama ya rangi ya kijani iliyotolewa na Marekani, Tel Aviv nayo kama alivyofanya mshirika wake mkongwe huyo, haikuwa na budi ila kukubali ukweli wa mambo na kwa hivyo imekiri rasmi kwamba suala la kuangushwa Damascus na serikali ya Bashar al-Asad halina maana tena.

Safari ya karibuni ya Abdallah bin Zayed Aal Nahyaan nchini Syria

Gazeti la Kiibrania la Israel Hume, limeandika kuwa, matukio ambayo yamekuwa yakitokea huko Syria katika siku za karibuni ni makubwa. Baada ya kupitisha kwa mafanikio kipindi kigumu cha vita vya ndani vilivyodumu kwa karibu muongo mmoja, sasa rais wa Syria anafanya juhudi kubwa kwa ajili ya kudhibiti ardhi yote ya nchi hiyo.

Tunaweza kusema kwamba baada ya kupata ushindi mkubwa katika mapambano na magaidi, Syria sasa inaendelea kupata mafanikio mengine muhimu katika uwanja wa siasa na diplomasia. Iwapo nchi kama Marekani, Saudi Arabia na Uturuki zitaacha siasa za chuki na njama za kuvuruga shughuli za serikali halali ya Syria ni wazi kuwa nchi hiyo itapata fursa nzuri ya kushughulikia masuala mengine muhimu ya kitaifa, ikiwemo shughuli ya kubuni katiba mpya.

Tags