Nov 22, 2021 02:23 UTC
  • Onyo la makundi ya mapambano ya Iraq kuhusu kuondoka askari wa Marekani

Kufuatia uvumi unaoenezwa kuhusu kutotekelezwa ratiba ya kuondoka askari wa Marekani katika ardhi ya Iraq, makundi ya mapambano ya nchi hiyo yametoa onyo kali kuhusu jambo hilo.

Wanajeshi wa Marekani waliivamia Iraq mwaka 2003 kwa ajili ya kuung'oa madarakani mfumo wa kibaathi wa nchi hiyo uliokuwa ukiongozwa na Saddam Hussein. Wengi wa askari hao waliondoka nchini humo mwaka 2011 baada ya kutimiza wajibu wao. Pamoja na hayo, wanajeshi hao walirejea Iraq mwaka 2014 kwa ombi la serikali ya nchi hiyo kwa lengo la kuisaidia kukabiliana na magaidi wa Daesh ambao katika kipindi hicho walikuwa wameteka na kukalia thuluthi moja ya ardhi ya Iraq. Kwa kisingizio hicho Marekani ilituma Iraq maelfu na malefu ya wanajeshi chini ya mwavuli wa muungano wa kimataifa kwa ajili ya kupambana na Daesh ambapo sehemu kubwa ya askari wa muungano huo walikuwa Wamarekani.

Baada ya kushindwa Daesh mwaka 2017, kuendelea kusalia Iraq askari wa Marekani uligeuka kuwa mjadala mkubwa kwa sababu hakukuwepo tena na sababu ya kuhalalisha kuendelea kusalia nchini humo askari hao vamizi. Hatua ya Marekani ya kumuua kigaidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (Sepah) na Abu Mahdi al-Muhandis, Naibu Mkuu wa Jeshi la Kujitolea la Wananchi wa Iraq la Hashdu-Sha'abi karibu na uwanja wa ndege wa Baghad, iliamsha hasira ya watu na makundi ya kisiasa ya Iraq, na hasa yale yanayofungamana na mrengo wa mapambano.

Makundi ya mapambano ya Iraq

Bunge la Iraq lilipitisha mswada wa kufukuzwa askari wote wa Marekani tarehe 5 Januari, ikiwa ni siku mbili tu baada ya kuuawa shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani. Tokea wakati huo kumekuwepo na mapigano na mivutano mingi kati ya makundi ya mapambano na askari vamizi wa Marekani. Hatimaye Mustafa al-Kadhimi, Waziri Mkuu wa Iraq na Rais Joe Biden wa Marekani tarehe 26 Julai mwaka huu walifikia mapatano ya kuondolewa askari wa nchi hiyo ya Magharibi katika ardhi ya Iraq. Kwa mujibu wa mapatano hayo, ilikubaliwa kuwa askari wote wapiganaji wa Marekani wanapaswa kuondoka Iraq kufikia mwishoni mwa mwaka huu na wale watakaoruhusiwa kubaki ni wale tu wanaotoa mafunzo na ushauri wa kijeshi kwa askari wa Iraq.

Huku zikiwa zimebaji chini ya siku 40 kabla ya kuondoka rasmi askari wa Marekani huko Iraq, uvumi umekuwa ukienezwa kwamba sasa ratiba ya kuondoka askari hao haitatekelezwa. Baadhi ya maafisa wa kijeshi wa Marekani akiwemo Jenerali Kenneth McKenzie, Mkuu wa Kamandi Kuu ya Majeshi ya Marekani CENTCOM wanasema askari wa nchi hiyo kwa sasa hawatatoka Iraq na kuwa hilo ni kutokana na ombi la serikali ya Baghdad.

Harakati za kijeshi za Marekani huko Iraq katika siku za karibuni, ikiwa ni pamoja na kuhamishiwa zana za kijeshi za nchi hiyo ya Magharibi nchini Iraq, kutengwa pesa nyingi kwa shabaha ya kutekeleza miradi ya ujenzi wa majengo ya kambi ya kijeshi ya Marekani ya Ain al-Asad iliyoko magharibi mwa Iraq na matamshi ambayo yamekuwa yakitolewa na viongozi wa ngazi za juu wa kisiasa na kijeshi wa Iraq kuwa Iraq inaihitajia Marekani kwa ajili ya kukabiliana na ugaidi, yote hayo ni mambo yanayothibitisha kuwa kuna njama inayofanyika kwa ajili ya kuwabakisha wanajeshi wa Marekani Iraq na kwamba huenda ratiba ya kufukuzwa kwao nchini humo isitekelezwe kwa sasa.

Wananchi wa Iraq wakipinga uwepo wa Marekani nchini kwao

Kwa kutilia maanani matamshi, harakati na uvumi ambao umekuwa ukienezwa katika uwanja huo, kamati ya uratibu ya makundi ya mapambano ya Iraq imeonya kwamba makundi hayo yataanza kukabiliana na askari vamizi wa Marekani mara tu baada ya kumalizika muda waliopewa kuondoka nchini. Katika uwanja huo, Abu Alaa al-Wilai, Katibu Mkuu wa Kataib Sayyid as-Shuhadaa ametoa taarifa akisema milango yote ya kusajili wapiganaji wapya wa kujitolewa wa kundi hilo kwa ajili ya kukabilia na askari wa Marekani baada ya kumalizika muda wao wa kuwa Iraq imefunguliwa.

Kwa kutilia maanani tahadhari hiyo iliyotolewa na makundi ya mapambano ya Iraq, ni wazi kuwa iwapo mapatano ya Julai hayatatekelezwa, kuna uwezekano mkubwa wa kutokea mapigano ya silaha kati ya makundi hayo na askari vamizi wa Marekani, mapigano ambayo huenda yakawa makali zaidi kuliko yaliyoshuhudiwa huko nyuma.

Tags