Nov 22, 2021 08:10 UTC
  • Wananchi wa Bahrain wwandamana kuwaunga mkono wafungwa wa kisiasa

Wananchi wa Bahrain wameandamana wakiwaunga mkono wafungwa wa kisiasa wa nchi hiyo na kutoa wito wa kuachiliwa huru wafungwa hao.

Waandamanaji hao wakiwa wamebeba mabango na maberamu walisikika wakipiga nara dhidi ya utawala wa kifamilia wa Manama na kuutaka uwaachilie huru wafungwa wa kisiasa wanaoshikiliwa katika magereza ya utawala huo.

Waandamanaji hao wamelaani pia kimya cha jamii ya kimataifa kuhusiana na mateso na unyama unaofanywa na utawala wa Bahrain dhidi ya wananchi wa nchi hiyo wanaopaza sauti zao wakitaka demokrasia ichukue mkondo wake.

Wakati huo huo Jumuiya ya Kiislamu ya Bahrain ya al Wifaq imetangaza kuwa, vikosi vya usalama vya Bahrain jana vilimtia mbaroni  Ali Mehna mmoja wa wanaharakati wa kisiasa na kijamii.

Bahrain ni miongoni mwa mataifa yanayokiuka haki za binadamu

 

Wiki iliyopita pia vyombo vya usalama nchini Bahrain viliwatia mbaroni vijana wanne wa Kibahrain kwa madai ya kushiriki katika maandamano ya kupinga kuanzishwa uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Kizayuni wa israel.

Utawala huo wa kiimla umekuwa ukikandamiza wapinzani tangu ulipotumia mkono wa chuma mwaka 2011 kwa msaada wa Saudi Arabia kupambana na maandamano ya umma ya kupigania mageuzi.

Mbali na adhabu za vifungo, utawala wa Aal Khalifa umewafutia uraia pia mamia ya Wabahrain katika kesi zilizoendeshwa kwa umati na mahakama za utawala huo.

Kwa mujibu wa taasisi za kutetea haki za binadamu, hukumu za adhabu ya kifo zimeongezeka mno pia nchini humo katika muongo mmoja uliopita hasa tangu lilipoanza vuguvugu la Machipuo ya Kiarabu mwaka 2011.

Tags