Nov 22, 2021 12:01 UTC
  • Wayemen waandamana kulaani uungaji mkono wa US kwa wavamizi

Maelfu ya wananchi wa Yemen wamefanya maandamano katika mkoa wa Sa'ada,kaskazini magharibi mwa nchi kulaani hatua ya Marekani ya kuunga mkono muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia katika vita dhidi ya taifa hilo maskini la Kiarabu.

Maandamano hayo yamefanyika mapema leo Jumatatu chini ya kaulimbiu inayosema "Marekani ni mhusika mkuu wa mgogoro wa kijeshi na kiuchumi, na kuendelea vita na mzingiro nchini Yemen."

Waandamanaji hao waliokuwa wamebeba bendera za nchi yao wamesikika wakipiga nara za 'Uhuru', "Tunapinga Ubeberu wa Marekani' na 'Marekani shetani mkubwa.'

Naibu Gavana wa mkoa wa Sa'ada, Yahya Al-Hamran ambaye ameshiriki maandamano hayo amesema katika taarifa kuwa, uvamizi wa Marekani-Saudia ndani ya miaka saba iliyopita imepelekea kupigwa kwa mabomu mahospitali, shule na nyumba za Wayemen.

Wayemen katika maandamano makubwa ya kulaani uvamizi wa Saudia kwa msaada wa Marekani

Mapema mwezi huu, Mjumbe wa Baraza Kuu la Siasa la Yemen alisema kuwa, hatua ya Rais Joe Biden wa Marekani ya kuidhinisha mauzo ya makombora kwa Saudia inakinzana waziwazi na wito wa kuwepo suluhu na amani nchini Yemen na inaunga mkono muungano vamizi unaoendelea kufanya mashambulizi dhidi ya watu wa Yemen.

Hii ni baada ya Wizara ya Ulinzi ya Marekani kutangaza kwamba, Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo imeafiki kuiuzia Saudi Arabia makombora 280 yenye thamani ya dola milioni 650. 

Hujuma na mashambulio hayo ya Saudia na washirika wake yanaendelea licha ya kuweko miito ya kieneo na kimataifa inayotaka kusitishwa mauaji hayo dhidi ya wananchi wa Yemen.

Tags