Nov 24, 2021 02:28 UTC
  • Kongamano la usalama la Manama; kutokuwa na natija mikutano ya usalama kama hii kwa ajili ya eneo la Asia Magharibi

Kongamano la 17 la usalama wa Asia Magharibi linalojulikana kama Mazungumzo ya 2021 ya Manama lilimalizika hivi karibuni nchini Bahrain.

Mazungumzo hayo ya 17 ya kila mwaka ambayo ni kongamano la usalama lenye umuhimu wa kiwango cha chini na taathira finyu katika nidhamu ya usalama wa eneo la Magharibi ya Asia yalianza Ijumaa iliyopita ya tarehe 19 na kumalizika siku ya Jumapili tarehe 21 mwezi huu. Historia ya kufanyika kongamano hili inarejea Disemba 2014 yaani mwaka mmoja baada ya kuvamiwa na kukaliwa kwa mabavu Iraq na majeshi vamizi ya Marekani pamoja na washirika wake.

Katika kongamano hili, mbali na kushiriki mataifa ya eneo la Asia Magharibi na nje ya eneo hili, hushiriki pia wawakilishi wa asasi za kieneo na kimataifa kama Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi {NATO}, Jumuiya ya Nchi za Kusini Mashariki mwa Asia {ASEAN}, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu {Arab League} na Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi. Kongamano la mara hii la Mazungumzo ya Manama lilianza kwa hotuba ya Lloyd James Austin, Waziri wa Ulinzi wa Marekani. Taswira ya mkutano huu ni kwamba, kivitendo hauna taathira ya kiusalama kwa nidhamu ya eneo la Asia Magharibi na kimsingi umejikita katika misimamo ya kisiasa pasi na kuwa na utendaji wa kiusalama. Hata mkutano wa mara hii nao umeendelea kufuata mkondo ule ule wa kutokuwa na taathira ya kuhisika kwa mwenendo wa usalama wa eneo hili.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Waziri wa Ulinzi wa Marekani alitoa matamshi yaliyo dhidi ya Iran. Lloyd Austin alitumia msamiati wa "ni jambo la kutumia machaguo yote" dhidi ya Iran na kudai kwamba, serikali ya nchi yake itaendelea kufungamana na matokeo ya mazungumzo ya kidiplomasia. Aidha alisema kuwa, "endapo Iran haitaonyesha nia ya dhati ya ushirikiano", wakati huo tutazingatia machaguo yote kwa shabaha ya kulinda usalama wa Marekani." Matamshi hayo yanatolewa katika hali ambayo, duru ya saba ya mazungumzo ya Vienna Austria imepangwa kufanyika tarehe 29 mwezi huu wa Novemba ikiwa ni duru ya kwanza ya mazunguzo hayo ya nyuklia tangu ilipoingia madarakani serikali mpya nchini Iran chini ya uongozi wa Dakta Ibrahim Raeisi.

 

Kwa msingi huo kuna mitazamo mitatu kuhusiana na matamshi ya Waziri wa Ulinzi wa Marekani. Mtazamo wa kwanza ni kuwa, Lloyd Austin kwa kutoa matamshi hayo wakati huu ametuma risala hasi kwa mazungumzo yajayo. Mtazamo mwingine ni kuwa, kabla ya kila kitu, matamshi hayo ni marhamu na pozo kwa washirika wa Marekani. Mtazamo wa tatu ni kuwa, Waziri wa Ulinzi wa Marekani alitaka kuzifikishia ujumbe nchi za eneo ambazo ni washirika wake wa eneo kwamba, Washington ingali inafungamana na suala la kulinda usalama wa nchi hizo.

Matamshi dhidi ya Iran hayakuishia kutolewa tu na Waziri wa Ulinzi wa Marekani. Baadhi ya viongozi walioshiriki katika kongamano hilo la Mazungumzo ya Manama nao walijitokeza na kuishambulia kwa maneno Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ahmed Aboul Gheit, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ni miongoni mwa viongozi waliokariri madai kwamba, Iran inaingilia masuala ya ndani ya nchi za Kiarabu. Abdullatif bin Rashid Al-Zayani, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Bahrain naye alifuata mkumbo na kuituhumuu Iran kwamba, eti inavuruga amani na usalama wa eneo la Asia Magharibi.

Fauka ya hayo, katika Kongamano la Mazungumzo ya Manama 2021, washiriki wa mkutano huo walionyesha msimamo ulio dhidi ya Serikali ya Wokovu  wa Kitaifa ya Yemen na kuituhumu Harakati  ya Wananchi ya  Ansarullah ya Yemen kwamba, eti inavuruga amani na usalama wa Yemen na wa eneo kwa ujumla. Kichekesho na kioja cha mwaka ni kuwa, wazungumzaji hao hawakuashiria hata kwa mbali mauaji ya kikatili na jinai zinazofanywa na utawala wa Saudi Arabia dhidi ya wananchi wa Yemen.

Maandamano ya wananchi wa Bahrain ya kupinga mkutano wa Manama, ambapo moja ya beramu la waandamanaji hao limeandikkwa: Mazungumzo ya Manama; uongo mtupu, hawajui isipokuwa lugha ya mauaji na kufungwa watu jela.

 

Ni kwa kuzingatia ukweli huu ndio maana wajuzi wa mambo wanaaamini kuwa, Kongamano la Mazungumzo ya Manama halina maana na wala mikutano ya usalama ya namna hii iliyojaa undumakuwili na matashi ya kisiasa haiwezi kuwa na natija yoyote ile kwa eneo la Asia Magharibi.

Wigo mwingine wa kuwa wa kisiasa mkutano wa Manama ni kushiriki katika kongamano hilo ujumbe kutoka Israel na kutumia mkutano huo kama jukwaa la kupigia upatu na kufuatilia suala la kudumishwa mwenendo wa kuanzishwa uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel.

Nukta ya mwisho ni kuwa matamshi ya washiriki wa mkutano wa usalama wa Manama yanaonyesha kuwa, kongamano hilo limegubikwa na matashi ya kisiasa na halina kabisa maana wala faida yoyote kwa usalama wa eneo la Asia Magharibi. Washiriki wa mkutano huo siyo tu kwamba, hawakulingatia na kulipa umuhimu suala la Palestina, bali kivitendo, mkutano huo umegeuzwa na kuwa uwanja wa kudhamini malengo ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel.

Tags