Nov 24, 2021 16:01 UTC
  • Mrithi wa ufalme wa Saudia apendekeza kulinunua shirika la Israel linalojihusisha na ujasusi

Duru moja katika ofisi ya ufalme wa Saudi Arabia imetangaza kuwa, mrithi wa ufalme wa nchi hiyo Mohammad bin Salman ametoa pendekezo la kulinunua shirika la utawala haramu wa Kizayuni linalojihusisha na ujasusi la NSO ambalo linakaribia kufilisika.

Kwa mujibu wa duru hiyo, Bin Salman anaonyesha kuwa na hamu kubwa ya kuwekeza katika masuala ya usalama wa intaneti na kupanua uwezo wa Saudia katika shughuli za ujasusi na udukuzi na anahisi shirika la NSO ni fursa adhimu ya kutimizia ndoto yake hiyo.

Miezi mitano nyuma, gazeti la kizayuni la Yediot Ahronot lilifichua kuwa, baada ya kuuliwa mkosoaji wa utawala wa Aal Saud Jamal Khashoggi katika ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul, Uturuki, wizara ya intelijensia ya Israel ilitoa idhini kwa shirika la NSO na mashirika mengine kadhaa ya kijasusi yatengeneze na kuipatia Riyadh vifaa na zana za ujasusi.

Gazeti hilo liliongeza kuwa, aidha Tel Aviv iliyaruhusu kwa njia ya siri mashirika yanayohusika na uangalizi wa kielektroniki kuendesha shughuli zao kwa manufaa ya Saudi Arabia.

Bin Salman na Netanyahu

Kwa mujibu wa gazeti la New York Times linalochapishwa Marekani, Mohammad Bin Salman ameshawahi kukutana kwa siri na aliyekuwa waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni Benjamin Netanyahu; na maafisa wa intelijensia wa pande hizo mbili pia wamekuwa wakikutana kwa utaratibu maalumu.

Gazeti la kizayuni la Haaretz nalo pia liliwahi kuripoti huko nyuma kwamba, tangu mwaka 2019 shirika la Israel la Quadrem limekuwa likiiuzia Saudia vifaa vya kisasa vya ujasusi.../

Tags