Nov 24, 2021 16:57 UTC
  • Makamanda wawili wa usalama Iraq wakamatwa kuhusiana na jaribio la kumuua waziri mkuu

Afisa mmoja wa jeshi nchini Iraq ametangaza kuwa, makamanda wawili wa usalama wametiwa nguvuni kuhusiana na njama na jaribio la kumuua waziri mkuu Mustafa al-Kadhimi.

Afisa huyo wa jeshi la Iraq amesema, Sabah Ash-Shibli, Murugenzi Mkuu wa kupambana na mada za miripuko katika wizara ya mambo ya ndani na afisa mmoja mwingine wamekamatwa ili kuhojiwa na kamati maalumu inayohusika na uchunguzi wa jaribio la kumuua waziri mkuu wa nchi hiyo Mustafa al-Kadhimi.

Kwa mujibu wa afisa huyo, sababu ya kukamatwa makamanda hao wa usalama ni kuharibu nyaraka na ushahidi kabla ya kuchukuliwa alama za vidole na kufanyika uchunguzi katika mahali lilipofanyika jaribio la kutaka kumuua al-Kadhimi.

Mustafa al Kadhimi

Awali kabla ya hapo, duru moja ya usalama ilitangaza kuwa, vikosi vya usalama vya Iraq vimewakamata watu watatu kuhusiana na njama ya kumuua waziri mkuu wa nchi hiyo tarehe 7 ya mwezi huu wa Novemba.

Katika jaribio hilo, ilielezwa kuwa ndege zisizo na rubani zilizosheheni mada za miripuko zililenga makazi ya kiongozi huyo katika mji mkuu Baghdad.

Hata hivyo al-Kadhimi alinusurika katika jaribio hilo.../