Nov 25, 2021 07:37 UTC
  • Safari ya mrithi wa ufalme wa Imarati nchini Uturuki; sababu na malengo yake

Mohammed Bin Zayed Al Nayhan, mrithi wa ufalme wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) jana Jumatano tarehe 24 Novemba aliwasili mjini Ankara, Uturuki ambapo alikutana na kufanya mazungumzo na Rais Recep Tayyip Erdoğan wa nchi hiyo.

Kuna nukta kadhaa za kuzingatiwa kuhusiana na safari ya Mohammed Bin Zayed nchini Uturuki:

Nukta ya kwanza ni kwamba, safari hiyo inaonyesha mabadiliko katika sera za nje za Imarati. Mnamo mwezi huu huu wa Novemba, Abdullah Bin Zayed, Waziri wa Mambo ya Nje wa Imarati alieleka Damascus, Syria ambapo alikutana na kufanya na mazungumzo na rais wa nchi hiyo Bashar al-Assad. Naye Mohammed Bin Zayed, kabla ya safari yake ya Uturuki, alikuwa ameshafanya mazungumzo na Erdogan kwa njia ya simu. Miezi mitatu nyuma, Tahnun Bin Zayed, mshauri wa usalama wa taifa wa Umoja wa Falme za Kiarabu, naye pia alifanya safari ya kuitembelea Uturuki. Mabadiliko yanayofanywa katika sera za nje za Imarati ni ushahidi wa imani waliyopata na hitimisho walilofikia viongozi wa Abu Dhabi kwamba sera za nje za kuleta suluhu ndizo zenye taathira chanya kwa ajili ya kuinua nafasi ya nchi hiyo.

Mohammed Bin Zayed na mwenyeji wake Erdogan baada ya kuwasili Ankara

Nukta ya pili kuhusu safari ya Mohammed Bin Zayed huko Uturuki ni kuwa, baada ya kupita kipindi cha miaka 10, hiyo ni safari yake ya kwanza aliyofanya kuelekea nchini humo. Tukio hilo limejiri wakati kuna mgongano wa wazi wa kiutambulisho baina ya Uturuki na Imarati. Serikali ya Uturuki inabeba utambulisho wa harakati ya Ikhwanul Muslimin na inajaribu kujenga na kueneza mfumo wa Kiikhwani katika eneo la Asia Magharibi. Lakini kwa upande wa Imarati, nchi hiyo ni mmoja wa wapinzani wakubwa wa Ikhwanul Muslimin, mpaka imefika hadi ya kuitangaza harakati hiyo kuwa ni kundi la kigaidi.

Katika miaka ya karibuni, kutokana na jinsi Imarati ilivyoamiliana na harakati ya Ikhwanul Muslimin, mivutano na mikwaruzano imezuka baina yake na Uturuki, huku Abu Dhabi ikionyesha upinzani wa waziwazi dhidi ya kujipenyeza na kuwa na ushawishi Ankara katika Ulimwengu wa Kiarabu. Sambamba na hilo, Umoja huo wa Falme za Kiarabu umeikosoa mara kadhaa pia Uturuki kwa kuiunga mkono Qatar. Lakini si hayo tu, wakati Uturuki ilikosoa na kulaani mapinduzi yaliyofanywa na wanajeshi dhidi ya serikali ya Ikhwanul Muslimin ya Misri iliyoongozwa na hayati Muhammad Morsi, Imarati iliunga mkono kikamilifu hatua hiyo. Aidha, wakati Uturuki inaunga mkono Ikhwanul Muslimin nchini Libya na inapinga Khalifa Haftar kushika hatamu za utawala, Imarati ikishirikiana na Saudi Arabia ni miongoni mwa waungaji mkono wa jenerali huyo mwasi na wanataka ashike madaraka ya nchi.

Erdogan (kulia) na hayati Morsi

Tofauti hizo zinaonyesha kuwa, kwa kuchukua hatua ya kufufua uhusiano wake na Uturuki, Imarati haiwezi kushirikiana na kwenda sambamba na sera za Ankara, na kwamba kuchukua hatua hiyo kumefanyika zaidi kwa lengo la kupunguza kiwango cha mivutano katika sera zake za nje; mivutano ambayo imeshtadi, hasa katika muongo huu wa karibuni, kutokana na hulka ya kupenda jaha na kutaka kuwa na sauti ya juu, ambayo imekuwa nayo Imarati na hasa mrithi wake wa ufalme Mohammed bin Zayed na uingiliaji wake katika masuala ya nchi nyingine, sambamba na kujaribu kutunishiana misuli na madola kama Uturuki na Iran. Kwa hivyo safari hiyo na ile ya nchini Syria zinaonyesha kuwa, Imarati imefikia himitisho la kwamba, haitaweza kujidhaminia maslahi yake kwa njia ya kuvutana na madola muhimu ya eneo pamoja na wadau wenye nafasi athirifu kama Syria.

Bashar al-Assad (kulia) na Abdullah Bin Zayed walipokutana hivi karibuni mjini Damascus

Na nukta ya tatu ni kwamba, moja ya malengo muhimu zaidi ya safari ya Mohammed Bin Zayed nchini Uturuki ni kutaka kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na nchi hiyo. Imarati inajaribu kuimarisha uhusiano wake na Uturuki kupitia kuwekeza mitaji nchini humo. Ukweli ni kwamba, Umoja wa Falme za Kiarabu unataka kujidhaminia maslahi yake ya kisiasa hasa katika eneo kupitia satua na ushawishi wa kiuchumi. Katika muelekeo huo, mwanzoni mwa mwezi huu wa Novemba imefunguliwa njia ya kupitishia bidhaa kutoka Uturuki kuelekea Imarati kupitia Iran, ambapo sasa usafirishaji bidhaa baina ya nchi mbili, uliokuwa ukichukua muda wa siku 20 kupitia njia ya baharini ya Mfereji wa Suez, utachukua muda wa siku sita hadi nane tu na kuwa na taathira kubwa katika kustawishwa uhusiano wa nchi mbili.

Na nukta ya kumalizia ni kwamba, kupitia uhusiano wake na Uturuki, kufufua uhusiano na Syria na kufanya mazungumzo na Iran, Imarati inadhamiria pia kuingia kwenye mchuano na Saudi Arabia na Qatar.../

 

 

Tags