Nov 25, 2021 14:32 UTC

Shirika la Polisi la Kimataifa (Interpol) limemteua Jenerali wa Imarati aneyetuhumiwa kutesa watu kuwa mkuu wake mpya kufuatia mkutano wake wa kila mwaka uliofanyika mjini Instanbul Uturuki.

Meja Jenerali Ahmed Naser al-Raisi, Inspekta Jenerali katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) ameteuliwa kuongoza shirika hilo kwa kipindi cha miaka minne, licha ya upinzani mkali ambao umekuwa ukielekezwa dhidi yake katika miezi ya hivi karibuni.

Mashirika mbalimbali ya kutetea haki za binadamu yanamtuhumu mkuu huyu mpya wa Polisi ya Kimataifa (Interpol) kwamba, amehusika na vitendo vya mateso na kuwakamata watu kiholela katika nchi yake ya Umoja wa Falme za Kiarabu.

Wanaokosoa uteuzi wake wanasema kuwa, jenerali huyo amekuwa akisimamia moja kwa moja jeshi la polisi la Imarati, ambalo lina faili jeusi la utendaji kazi, kwa kukiuka sheria na haki za binadamu.

Polisi ya Kimataifa (Interpol)

 

Hivi karibuni shirika huru la kutetea haki za binadamu la Persian Gulf Center for Human Rights (GCHR) lenye makao makuu yake mjini London, Uingereza liliwasilisha malalamiko katika mahakama moja ya Paris nchini Ufaransa, dhidi ya Meja Jenerali al-Raisi, Inspekta Jenerali katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Imarati.

Aidha makumi ya Wabunge wa Ufaransa wamewahi kulalamikia huko nyuma hatua ya kutaka  kuteuliwa afisa huyo wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kuwa Mkuu wa Polisi ya Kimataifa (Interpol).

Katika barua yao mwezi Juni mwaka huu watunga sheria hao walionya kuwa, Meja Jenerali Ahmed Naser al-Raisi ana rekodi ndefu ya ukiukaji wa haki.

Tags