Nov 26, 2021 02:48 UTC
  • Marekani yaendeleza njama za umwagaji damu ili kuhakikisha haitimuliwi nchini Iraq

Makundi ya kisisa nchini Iraq yamesema kuwa, Marekani inaendelea kufanya njama za kuchochea machafuko na umwagaji damu nchini Iraq ili kujiwekea kinga ya kutotimuliwa nchini humo.

Tovuti ya habari ya al Maaluma imemnukuu Faris Shakir, mjumbe wa muungano wa Fat'h nchini iraq akisema kuwa, Marekani inaendesha njama za kuzusha fitna, machafuko na mauaji nchini Iraq ili kushinikiza kubakia wanajeshi nchini humo na kutengwa kila anayepigania kutimuliwa wanajeshi magaidi wa Marekani huko Iraq.

Naye Mohammad al Sahyud, mjumbe wa muungano wa Serikali ya Sheria nchini Iraq amesema, Iraq hivi sasa haihitaji tena kuweko wanajeshi wa Marekani nchini humo na kila mmoja anajua vyema uamuzi wa Bunge na makubaliano ya kutimuliwa wanajeshi wa Marekani nchini Iraq ifikapo mwishoni mwa mwaka huu wa 2021. Kwa kweli hakuna kitu chochote kinachoweza kuhalalisha kuendelea kuweko wanajeshi wa Marekani nchini Iraq.

Marekani imemimina wanajeshi wake nchini Iraq eti kwa ajili ya kuimarisha demokrasia

 

Kwa upande wake, Muhsin al Saidi, mjumbe wa Harakati ya Sheria ya Iraq amesema, Marekani hivi sasa inaendeleza njama za kuhakikisha inabakia nchini Iraq kwa gharama zozote zile, wakati ambapo wanaoshiriki kwenye njama hizo za Marekani hawalitakii kheri ya aina yoyote taifa la Iraq.

Kwa mujibu wa muswada uliopasishwa na Bunge la Iraq, wanajeshi magaidi wa Marekani wanapaswa waondoke nchini humo ifikapo mwishoni mwa mwaka huu wa 2021. Hata hivyo kwa muda sasa Marekani imekuwa ikifanya njama za kila namna za kuzusha fitna, fujo na uhalifu wa umwagaji wa damu ili kuhakikisha haitimuliwi katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Tags