Nov 26, 2021 12:03 UTC
  • Uhusiano wa Iran na UAE uko katika mkondo wa kuboreka

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anayeshughulikia masuala ya kisiasa amesema kumefikiwa mapatano na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kwa lengo la kuboresha uhusiano wa nchi hizi mbili.

Ali Bagheri Kani siku ya Jumatano alitembelea UAE ikiwa ni muendelezeo wa safari katika nchi za eneo ambapo akiwa Dubai alikuwa na mkutano wa kirafiki na  Anwar Gargash mshauri wa ngazi za juu wa Rais wa UAE na Waziri Mashauri wa Mambo ya Kigeni Khalifa Shaheen Almarar. Baada ya kikao hicho, Bagheri Kani amesema kumefikiwa mapatano ya kufungua ukurasa mpya katika uhusiano wa Iran na UAE.

Kauli za wakuu wa Iran na UAE katika miezi ya hivi karibuni zinaonyesha kuwa pande mbili zina hamu ya kuboresha uhusiano hasa katika nyuga za uchumi na biashara. Nchi hizi mbili jirani katika Ghuba ya Uajemi zina historia ndefu ya ushirikiano ambao umekuwa na pandashuka za kisiasa lakini uhusiano wa kiuchumi haujawahi kusitishwa.

Baada ya kuanza kutekelezwa vikwazo vipya vya Marekani sambamba na kushinikziwa nchi za eneo kupunguza uhusiano na Iran, kulishuhudiwa kupungua uhusiano wa kibiashara baina ya Iran na UAE. Pamoja na hayo kutegemeana kiuchumi kumefanya nchi hizi mbili kuchukua msimamo wa wastani na hivyo zinajitahidi kuimarisha ushirikiano. Kwa maneneo mengine ni kuwa, uhusiano wa kiuchumi ni nukta muhimu zaidi  inayozifungamanisha nchi hizi mbili na kwa msingi huo, hata katika mazingira mabaya zaidi ya vikwazo na kudororoa uhusiano wa kisiasa, UAE imebakia kuwa miongoni mwa nchi tano washirika wakubwa zaidi wa kibiashara wa Iran.

Dubai

Biashara baina ya Iran na UAE au Imarati katika miezi ya kwanza  mitano ya mwaka mpya wa Kiirani 1400 ulioanza Machi 21 imefikia dola bilioni 7.3. Idadi hiyo ikilinganishwa na wakati kama huo mwaka mmoja uliopita inaonyesha ongezeko la thamani yake kwa asilimia 54.

Kipaumbele cha Iran katika masuala ya kisiasa, kiusalama na kiuchumi ni kuwa na uhusiano mwema na nchi jirani na kama wanavyosema wakuu wa Imarati, nchi mbili zinajitahidi kupunguza taharuki katika eneo.

Anwar Gargash Mshauri wa Rais wa UAE katika masuala ya kigeni akizungumza katika 'Kongamano la  Sera za Kimataifa Dubai' alisema nchi yake inalenga kupunguza taharuki na mashindano baina yake na Iran pamoja na Uturuki ili kuondoa uwezekano wa makabiliano mapya katika eneo.

UAE inahesabiwa kuwa kituo muhimu cha kuuza bidhaa za Iran katika soko la kimataifa na nukta hiyo imepelekea wafanyabiashara wengi wa Iran kuendesha shughuli zao na kuwekeza katika nchi hiyo hasa mjini Dubai.

Hivi sasa kuna pendekezo la kufikisha bidhaa za UAE barani Ulaya kupitia njia ya Iran na Uturuki na bila shaka jambo hilo ni kwa maslahi ya nchi hizo tatu. Kadhia hiyo sasa inafuatiliwa kwa karibu na wakuu wa nchi husika na hivi karibuni kutazinduliwa korido ya UAE-Iran-Uturuki.

Ni wazi kuwa maslahi ya kisiasa, kiuchumi na kiusalama ya Iran na Imarati kama nchi mbili jirani yako katika kuimarisha uhusiano wa pande mbili na pia uhusiano wa kieneo. Nchi zote mbili zinasisitiza umuhimu wa kuimarishwa uhusiano wa kisiasa, ujirani mwema na kuheshimiana na pia zinajitahidi kuleta uthabiti na ustawi wa kiuchumi katika eneo sambamba na kukuza ushirikiano wa kibiashara na kiuchumi.

Ni kwa msingi huu ndio uhusiano wa kidiplomasia na kibiashara baina ya nchi mbili ukaimarika sana katika miezi ya hivi karibuni na inatabiriwa kuwa ushirikiano wa pande mbili utaimarika siku za usoni katika uga wa kiuchumi.

Mkutano wa hivi karibuni wa Ali Baqeri Kani na wakuu wa Imarati kwa ajili ya kufungua ukurasa mpya wa uhusiano umefanyika katika fremu hiyo hiyo ya matumaini kuhusu mustakabali.

Jamal al Fadhli mhadhiri wa sayansi ya kisiasa katika Chuo Kikuu cha Kuwait anasema hivi kuhusu uhusiano wa Iran na nchi za Kiarabu: "Si mantiki kuendelea kuwepo taharuki baina ya Iran na nchi za Kiarabu katika Ghuba ya Uajemi. Ushirikiano baina ya Iran na nchi hizi sambamba na kutumiwa uwezo wa kijeshi, kiuchumi na kibiashara wa Iran ni jambo la dharura kwa nchi za Kiarabu. Badala ya nchi za Kiarabu kutafuta himaya ya Marekani ambayo daima inalenga kutumia vibaya hali hiyo kwa maslahi yake ya kifedha, nchi hizi zinapaswa kushirikiana na Iran."