Nov 27, 2021 03:42 UTC
  • Australia inaitumikia Marekani na utawala wa Kizayuni

Serikali ya Australia imeiweka harakati ya Hizbullah ya Lebanon katika orodha ya eti makundi ya kigaidi sambamba na kuipiga marufuku harakati hiyo katika hatua ambayo inayonekana imechukuliwa ili kuihudumia Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Duru za Kimagharibi zinadokeza kuwa, baadhi ya madola ya Magharibi yameanza kuzidisha mashinikizo dhidi ya Hizbullah katika wiki za karibuni kwa lengo la kuitenga harakati hiyo. Hii ni katika hali ambayo, Hizbullah ni chama rasmi cha kisiasa ambacho kina viti katika Bunge la Lebanon.

Mbali na kuwa Harakati ya Hizbullah inakabiliana na utawala ghasibu na wa kibaguzi wa Israel, pia hutoa huduma na misaada ya kijamii, kiuchumi, na kiutamaduni kwa watu wa Lebanon. Hizbullah ina nafasi muhimu sana katika sekta ya kijamii nchini Lebanon. Kwa maelezo mengine ni kuwa, Hizbullah ni kati ya makundi ya kisiasa yenye taathira kubwa zaidi Lebanon na pia kijamii ina uungaji mkono mkubwa miongoni mwa wananchi.

Sayyid Jalala Saadatian, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anazungumza kuhusu kuongezeka mashinikizo dhidi ya Hizbullah katika nchi za Magharibi na kusema: 

"Duru zinazofungamana na madola ya Magharibi na zinazounga mkokono utawala wa Kizayuni wa Israel zinawasilisha madai yasiyo na msingi wowote dhidi ya Hizbullah, ambayo ni harakati yenye uwezo mkubwa Asia Magharibi ili kupunguza uungaji mkono na ushawishi wa kisiasa wa kundi hilo miongoni mwa wananchi.

Katibu Mkuu wa Hizbullah Sayyid Hassan Nasrallah

Ingawa kuna makundi mengine mbali mbali na maarufu katika uga wa kisiasa Lebanon, lakini Hizbullah ina umashuhuri mkubwa zaidi miongoni mwa wananachi. Nukta hii inaonyesha kuwa Hizbullah ina sifa za kipekee ambazo zimepelekea iungwe mkono na wananchi wengi Lebanon na moja ya sifa hizo ni ushujaa wa kundi hilo katika kuuzuia utawala wa Kizayuni wa Israeli usiteke ardhi ya Lebanon. Nukta hii imeifanya Hizbullah ipendwe na watu wa matabaka na dini mbali mbali nchini humo.

Ukweli ni kwamba, Hizbullah imepata nguvu na uwezo mkubwa kutokana na uungaji mkono wa wananchi wa Lebanon na nukta hiyo imepelekea harakati hiyo kupata umaarufu pia katika ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu.

Hassan Hanizadeh, mtaalamu wa masuala ya Asia Magharibi anabainisha nukta hii kwa kusema: "Kumeshuhudiwa ongezeko la mashinikizo  ya madola ya Magharibi na waitifaki wake dhidi ya Hizbullah kwa kutumia mbinu mbali mbali kwa lengo la kuidhoofisha harakati hii miongoni mwa wananchi wa Lebanon. Hizbullah ambayo ni harakati ya wananchi inashinikizwa na kudhoofishwa ili kuupa nguvu utawala wa Kizayuni na kuficha mapigo ambayo utawala huo umeyapata katika makabiliano na Hizbullah katika miaka ya karibuni.

Wapiganaji wa Harakati ya Hizbuallah

Kwa vyovyote vile, Marekani inaendeleza uungaji mkono wake kwa utawala wa kibaguzi wa Israel huku ikizidisha mashinikizo yake dhidi ya Hizbullah ambayo inaungwa mkono kikamilifu na watu wa Lebanon. Wananchi wa Lebanon wanaitambua Hizbullah kama harakati ambayo inakabiliana na jinai pamoja na ukoloni wa utawala ghasibu wa Israel. Hivyo kwa Walebanon waliowengi si tu kuwa Hizbullah si kundi la kigaidi bali wanajifakharisha nayo na kwa msingi huo hatua kama ile iliyochukuliwa na utawala wa Australia  haiwezi kuteteresha nafasi ya Hizbullah nchini Lebanon.