Nov 27, 2021 08:02 UTC
  • Wananchi wa Jordan waandamana kupinga kuanzishwa uhusiano wa kawaida na Israel

Mamia ya wananchi wa Jordan wameandamana wakilalamikia mwenendo wa mataifa ya Kiarabu wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel unaotenda jinai kila uchao dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina.

Waandamanaji hao wakiwa wamebeba mabango na maberamu wamelaani hatua yoyote ile ya kutaka kuanzisha uhusiano na utawala ghasibu wa Israel.

Aidha waandamanaji hao wamepinga vikali makubaliano ya nchi yao na utawala vamizi wa Israel ya kubadilishana nishati ya umeme na maji.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, safari ya Benny Gantz Waziri wa Vita wa utawala dhalimu wa Kizayuni wa Israel huko Morocco nayo imekabiliwa na upinzani mkali pamoja na maandamano ya wananchi ambao wametangaza wazi kupinga hatua ya serikali ya Rabat ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Bahrain na Imarati walipofikia makubaliano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel Septemba 2020.

 

Itakumbukwa kuwa, Septemba mwaka jana (2020), Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Imarati na Bahrain walisaini mkataba wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel katika hafla iliyofanyika Ikulu ya White House mjini Washington.

Baada ya hapo Sudan na Morocco nazo zikafuata mkumbo huo huo na kutangaza  kuanzisha uhusiano na utawala huo haramu, uamuzi ambao umeendelea kulalamikiwa na kulaaniwa na wapenda haki kote ulimwenguni.

Sudan, Morocco na Bahrain zimeendelea kushuhudia maandamano kila leo ya kulaani na kupinga hatua ya nchi zao ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa  Israel, wakisema kuwa, hatua hiyo ni khiyana na usaliti mkubwa kwa wananchi wa Palestina wanaofanyiwa unyama wa kila aina na utawala huo kila uchao.