Nov 28, 2021 02:50 UTC
  •  Taliban yaituhumu CIA kuwa inafanya mipango ya kuigawa Afghanistan

Afisa wa ngazi ya juu wa kundi la Taliban ametangaza kuwa Shirika la Ujasusi la Marekani CIA linafanya jitihada za kuigawa Afghanistan.

Anas Haqqani pia ameitaja Marekani kuwa chanzo kikuu cha mgogoro wa Afghanistan. 

Matamshi ya afisa huyo wa ngazi ya juu wa kundi la Taliban linaloongoza Afghanistan yametegemea mtazamo kwamba, katika zama zilizopita za utawala wa Afghanistan yaani wakati wa uongozi wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Ashraf-Ghani, baadhi ya makamanda wa jeshi la Marekani walikuwa wakiamini kuwa Afghanistan inapasa kugawanywa kwa mujibu wa jiografia ya makabila ya nchi hiyo ili kuweza kupata ufumbuzi mgogoro wa nchi hiyo na kwamba kila eneo linapasa kuwa utawala wake. 

Ashraf Ghani Rais wa Afghanistan aliyeikimbia nchi 

Wakati huo huo baadhi ya duru pia zimezungumzia suala la kuasisiwa utawala wa shirikisho huko Afghanistan. Baadhi ya mirengo ya kisiaa ndani ya nchi hiyo pia yalisisitiza mtazamo wa kubadilishwa muundo wa kisiasa wa Afghanistan kutoka muundo wa urais hadi utawala wa kibunge na kusema kunaweza kutatua matatizo ya nchi hiyo. Hata hivyo makubaliano yaliyosainiwa huko Doha nchini Qatar kati ya Marekani na kundi la Taliban wakati wa utawala wa rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump,  baada ya miezi 18 ya mazungumzo ya vuta nikuvute kati ya pande mbili, yaliandaa mazingira ya kundi la Taliban kuidhibiti tena Afghanistan na kuzuia utekelezaji wa mipango na masuala mengine kwa ajili ya mustakbali wa kisiasa wa Afghanistan.   

Vahid Mujde aliyekuwa mchambuzi wa masuala ya kisiasa nchini Afghanistan anaamini kuhusiana na suala hilo kuwa: Popote pale Marekani inaposhindwa kulikandamiza taifa fulani hufanya jitihada za kuligawa nchi hiyo. Kwa mtazamo huo, makubaliano ya Doha kati ya Marekani na kundi la Taliban pia yanstathminiwa kuwa ni katika jitihada za Washington za kutaka kuigawa Afghanistan.  

Hata hivyo  hitilafu zilizopo kati ya kundi la Taliban na Marekani kuhusu namna ya kuyatekeleza makubaliano hayo ya Doha ambapo inaonekana kuwa yamepelekea kutekwa na kushikiliwa mji mkuu, Kabul kutokana na mrengo wa Haqqani kuyapuuza makubaliano hayo, zimeifanya Marekani izuie fedha za Afghanistan na kwa njia hiyo iweze kuizidishia Taliban mashinikizo zaidi ili irejee kutekeleza makubaliano ya Doha.   

Kwa kuzingatia hali hii ya kutunishiana misuli kati ya Marekani na Taliban, mrengo wa Haqqani umeituhumu Marekani kuwa inafanya jitihada za kuigawa Afghanistan na kwa njia hiyo kuiweka Washington chini ya mashinikizo ya waliowengi ili ishirikiane na Taliban. Hii ni kwa sababu, mrengo huo unajua vyema kwamba, wenyewe ndio mlengwa wa mashinikizo ya Marekani kwa Taliban; na wakati huo huo mrengo wa Haqqani pia ambao unafanya kazi chini ya mwavuli wa Shirika la Intelijinsia la Jeshi la Pakistan (ISI), umeazimia kuimarisha pakubwa nafasi yake ndani ya Taliban kwa kukataa kushirikiana na Marekani katika makubaliano yaliyosainiwa Doha kati ya nchi hiyo na mrengo wa Mullah Baladar na hivyo kuzidisha nafasi yake ndani ya kundi hilo. 

Mullah Baladar 

Hii ni katika hali ambayo viongozi wengine wa Taliban wanataka kutambuliwa rasmi serikali ya kundi hilo huko Afghanistan; suala linalohitajia kupatiwa ufumbuzi hitilafu zilizopo ndani ya Taliban yenyewe na kuundwa serikali ya kitaifa na shirikishi na hivyo kuzuia visingizo vya aina yoyote kutoka kwa Marekani na mashirika yake ya kijasusi yanayoweza kutumiwa kwa ajili ya kuingilia masuala ya ndani ya Afghanistan. 

Abdulsattar Dushuki mchambuzi wa masuala ya kisiasa anaamini kuhusu hilo kwamba: Katika miongo kadhaa iliyopita Marekani ilifanya juu chini kuibua mivutano na hitilafu katika maeneo ya Wapashtu na katika maeneo ya Watajiki ambayo wakazi wake wengi wanazungumza lugha ya Kifarsi na pia kuibua mivutano na hitilafu katikati na kaskazini mwa Afghanistan katika maeneo ya Wauzbeki,  Waturkmeni na yale ya Wahazara. Marekani ilifanya hivyo lengo likiwa ni kuchochea chuki na uhasama wa kikabila na kidini katika maeneo hayo, fitina ambayo inaendelea hadi sasa; hivyo wananchi wa Afghanistan wanapasa kuwa macho mbele ya njama hiyo. 

Tags