Nov 28, 2021 08:03 UTC
  • Umoja wa Maulamaa Waislamu: Ni haramu kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni

Umoja wa Kimataifa wa Maulamaa Waislamu umelaani hatua ya baadhi ya nchi za Kiarabu ya kuanzisha muungano na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel na kusaini mikataba ya mapatano na utawala huo ghasibu.

Gazeti la al Quds al Araby limeripoti kuwa, Umoja wa Maulamaa Waislamu umetoa taarifa na kueleza kwamba miungano na hatua za kivitendo zilizochukuliwa na baadhi ya nchi za Kiarabu kwa ajili ya kuanzisha uhusiano na Israel ni tendo la kulaaniwa na ni usaliti dhidi ya watu wa Palestina.

Umoja wa Maulamaa Waislamu umetilia mkazo msimamo wake wa kuunga mkono Msikiti mtukufu wa Al Aqsa na Palestina na kulaani hatua ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Kizayuni itakayochukuliwa na nchi yoyote au kundi lolote lile.

Umoja huo vilevile umetaka zifanyike kila jitihada za kimaada na kimaanawi kwa ajili ya kuzikomboa ardhi zote zinazokaliwa kwa mabavu na hasa msikiti wa Al Aqsa na Quds tukufu.

Nchi nne za Kiarabu za Imarati (UAE), Bahrain, Morocco na Sudan mwaka uliopita wa 2020 zilisaini hati za makubaliano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel, hatua ambayo imepingwa na kulaaniwa vikali katika nchi za Kiarabu na Kiislamu.../ 

Tags