Nov 28, 2021 11:59 UTC
  • Onyo la HAMAS kwa rais wa utawala haramu wa Israel

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imetahadharisha kuhusu matokeo mabaya ya mpango wa Rais wa utawala wa Kizayuni wa Israel, Isaac Herzog wa kuutembelea Mstikiti wa Ibrahim kusini magharibi mwa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Ofisi ya Herzog ilitangaza Ijumaa kuwa, rais huyo wa utawala haramu wa Israel atautembelea Msikiti huo ambao ni moja ya maeneo matukufu na hasasi kwa Waislamu katika mji wa al-Khalil katika Ukingo wa Magharibi leo Jumapili, kushiriki matambiko ya Kiyahudi ya Hanukkah (hafla ya kuwasha mishumaa).

Ismail Radwan, afisa mwandamizi wa HAMAS amebainisha kuwa, utawala ghasibu wa Israel uwe tayari kubeba dhima ya chochote kitakachofanyika kutokana na chokochoko zake hizo mpya dhidi ya matukufu ya Kiislamu.

Wazayuni katika Msikiti wa Ibrahim mjini al-Khalil

Sanjari na kutoa mwito kwa Wapalestina wote kujitokeza kuzuia uafriti huo, afisa huyo wa ngazi ya juu wa HAMAS amesisitiza kuwa, sherehe hizo za kitamaduni za Wazayuni zinafanyika katika msikiti wa Waislamu kwa lengo la kuchochea hisia za Wapalestina, sambamba na kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu.

Amewataka Wapalestina wote kuzuia hujuma hiyo dhidi ya msikiti mtakatifu wa Ibrahim ulioko katika mji wa al-Khalil kusini mwa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan unaokaliwa kwa mabavu na utawala khabithi wa Israel.

Tags