Nov 29, 2021 14:00 UTC
  • Guterres: Hali ya mambo katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu Palestina inatishia amani

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, hali ya mambo katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu huko Palestina ni tishio kwa amani na uthabiti wa kiimataiifa.

Antonio Guterres amesema hayo leo kwa mnasaba wa Siku ya Kimataiifa ya Kufungamana na Wananchi wa Palestina ambapo sambamba na kuashiria uvamizi wa Israel huko Palestina amebainisha kwamba, hali ya mambo inayotawala katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu huko Palestina ni tishio la wazi kwa amani na usalama wa kimataifa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataiifa amesisitiza katika ujumbe wake aliouandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijami wa twitter kwamba: Wananchi wa Palestina wanapaswa kupata haki zao na kuwa na fursa ya kujenga mustakabali ambao utakuwa na amani na umoja.

Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa

 

Mwaka 1977 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliitangaza Tarehe 29 Novemba kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Kuonesha Mshikamano na Taifa la Palestina. Sababu ya hatua hiyo ni nafasi na mchango wa Baraza Kuu la umoja huo katika kuigawa ardhi ya Palestina.

Tarehe 29 Novemba 1947 baraza hilo lilipasisha azimio nambari 181 lililoidhinisha kugawanywa ardhi ya Palestina. Kwa mujibu wa azimio hilo Palestina iligawanywa sehemu mbili kwa ajili ya kuundwa dola la Kiyahudi na nchi ya Palestina.

Pamoja na hayo hadi sasa utawala ghasibu wa Israel haujawahi kuheshimu azimio hilo na daima umekuwa ukijitanua na kutwaa ardhi zaidi za Palestina kwa kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi iliyoghusubiwa.