Nov 30, 2021 04:30 UTC
  • Israel imewasababishia Wapalestina hasara ya dola bilioni 57 katika Ukingo wa  Magharibi

Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo UNCTAD limechapisha ripoti inayoonyesha kuwa sera za ukaliaji mabavu za utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan zimesababisha hasara ya kiuchumi ya zaidi ya dola bilioni 57 kwa taifa la Palestina katika kipindi cha miongo miwili iliyopita.

Katika miongo miwili ya kwanza ya karne ya 21, utawala wa Kizayuni umeendeleza sera zake za ukatili na utumiaji mabavu dhidi ya Wapalestina. Kwa ujumla, katika miongo miwili iliyopita, utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa ukifuatilia aina tatu za sera dhidi ya Palestina nazo ni vita, mzingiro na vikwazo au vizuizi.

Katika miongo miwili iliyopita, utawala wa Kizayuni wa Israel umeanzisha vita vya muda mrefu mara tatu na vita vya muda mfupi mara kadhaa na hali kadhalika oparesheni za kijeshi za kila siku dhidi ya Wapalestina.

Kuanzia mwaka 2000 hadi 2005 kulikuwa na Intifadha au mwamko wa Wapalestina ambapo katika kipindi hicho cha miaka mitano utawala wa Kizayuni ulikuwa unadondosha mabomu kila siku katika ardhi za Wapalestina. Mwaka 2008 utawala dhalimu wa Israeli ulitekeleza vita vya siku 22 mwaka 2012 vita vya siku 8, mwaka 2014 vita vya siku 51 na mwaka 2021 vita vya siku 12 dhidi ya Wapalestina. Aidha kila siku na kila saa Wapalestina wanakabiliwa na hujuma za mabomu ya utawala wa Israel.

Tokea mwaka 2006 hadi sasa, utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa ukitekeleza mzingiro wa pande zote dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza na kwa mujibu wa ripoti za Umoja wa Mataifa, Ghaza sasa imebadilika na kuwa gereza kubwa zaidi la wazi duniani.

Sera hizo za kuwawekea Wapalestina vizuizi zinatekelezwa katika fremu ya kuitenga Palestina kijiografia na kukata mawasiliano baina ya Wapalestina katika ardhi zote zinazokaliwa kwa mabavu. Vizuizi hivyo vimepelekea  ardhi zaidi za Wapalestina ziendelee kuporwa na utawala wa Kizayuni ambapo katika uporaji huo nyumba za Wapalestina hubomolewa kiholela na kuwasababishia hasara kubwa.

Hali kadhalika kuwekewa Wapalestina vizuizi vya kijiografia kumepelekea kupotea fursa za kiuchumi katika nchi hiyo inayokoloniwa hasa katika sekta ya kilimo ambapo Wakulima Wapalestina wamepata hasara kubwa.

Kwa kuzingatia sera hizi za mabavu za utawala wa Kizayuni wa Israel,  Richard Kozul-Wright Mkurugenzi wa Kitengo cha Maendeleo na Utandawazi katika UNCTAD anasema wanakadiria kuwa, sera za utawala haramu wa Israel zimepelekea kutoweka thuluthi moja ya Pato Ghafi la Ndani (GDP) la Palestina.

Sera za utawala wa Israel za vizuizi na vizingiti  dhidi ya Palestina sambamba na oparesheni za kijeshi za utawala huo katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan tokea mwaka 2000 hadi sasa zimewasababishia Wapalestina hasara ya kifedha na kiuchumi ya zaidi ya dola biloni 57.7.

Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa imeashiria tu sehemu ndogo ya hasara Wanayopata Wapalestina kutokana na sera za utawala haramu wa Israel kwani hasara kubwa waliyopata Wapalestina haijaashiriwa hata kidogo katika ripoti hiyo. Ripoti ya mwezi Novemba 2020 ya Umoja wa Mataifa ilibaini kuwa Ukanda wa Ghaza umepata hasara ya kiuchumi ya dola bilioni 1.7 kutokana na mzingiro wa Israel dhidi ya eneo hilo ambalo linakumbwa na umasikini mkubwa na ukosefu wa ajira.

Ripoti hizo za Umoja wa Mataifa hazijaashiria hasara kubwa ambayo Wapalestina wamepata kutokana na uharibifu uliosababishwa na vita ambavyo huibuliwa mara kwa mara na utawala huo wa Kizayuni.

Hali baada ya hujuma ya Israel dhidi ya eneo moja Ghaza

Vita viwe ni vya muda mrefu au vya muda mfupi hupelekea kuharibiwa miundo mbinu ya Wapalestina na hivyo kusababisha hasra kubwa. Iwapo tutakusanya pamoja hasara zote zinazopatikana kutokana na vita na mzingiro dhidi ya Wapalestina, basi hakuna shaka kuwa itabainika kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel umewasababishia Wapalestina hasara mara kadhaa zaidi ya iliyotangazwa.

Nukta muhimu ni hii kuwa, pamoja na kuwa Umoja wa Mataifa unakiri kuwa utawala haramu wa Israel umewasababishia Wapalestina hasara kubwa, lakini umoja huo haujachukua hatua zozote za kuzuia ukatili wa Israel dhidi ya taifa la Palestina. Uungaji mkono wa madola makubwa hasa Marekani na Uingereza kwa utawala wa Kizayuni wa Israel ni jambo ambalo limepelekea umoja huo ushindwe kuchukua hatua za kuwatetea Wapalestina.

Tags