Nov 30, 2021 07:54 UTC
  • OIC yamlaani rais wa Israel kwa kuingia Msikiti wa Ibrahim AS kinyume cha sheria

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imelaani hatua ya Rais Isaac Herzog wa utawala wa Kizayuni wa Israel kuingia kinyume cha sheria katika Msikiti wa Nabii Ibrahim AS katika mji wa Al Khalil au Hebron kusini mwa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Katika taarifa Jumatatu usiku, OIC imesema: "Kitendo hicho kimefanyika katika fremu ya mpango maalumu ulioratibiwa wa Kuyahudisha eneo hiilo na kushadidisha satwa ya utawala wa Kizayuni."

Hali kadhalika OIC imesema kitendo hicho cha rais wa utawala wa Kizayuni wa Israel kuingia kinyume cha sheria katika Msikiti wa Nabii Ibrahim AS kimelenga kuchochea hisia za Waislamu na ni muendelezo wa sera za kivamivi  za Israel sambamba na ukiukwaji wa haki, ardhi na matukifu ya Wapalestina.

OIC imeitaka jamii ya kimataifa kuunga mkono matukufu ya kidini na maeneo ya kihistoria na iwalazimu wakuu wa utawala wa Kizayuni kuheshimu maeneo hayo matakatifu. 

Jumapili usiku, Isaac Herzog, rais wa utawala wa Kizyuni wa Israel akiongoza Walowezi wa kizayuni alifika katika Msikiti wa Ibrahim AS huku akiwa chini ya ulinzi mkali. 

Wazayuni wakiwa wanahujumu na kuuvunjia heshima Msikiti wa Nabii Ibrahim AS

Msikiti wa Ibrahim AS ambao ni eneo takatifu kwa Waislamu na Mayahudi  ni Haram Takatifu na uko katika kitongoji cha kale cha Al Khalil (Hebron) kusini mwa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Kwa mujibu wa baadhi ya Hadithi, ndani ya msikiti huo kuna kaburi la Nabii Ibrahim AS na mkewe Sarah na vile vile makaburi ya Manabii Is-haq na Yaaqub AS na ya wake zao.

Itakumbukwa kuwa mnamo mwezi Julai mwaka 2017, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) lilitangaza kuwa mji wa Al Khalil ulioko Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan ambao ni moja ya turathi za kimataifa unakabiliwa na hatari kutokana na sera haribifu za utawala wa Kizayuni.

Tags