Nov 30, 2021 12:02 UTC
  • Syria: Tunaunga mkono kuundwa nchi huru ya Palestina mji wake mkuu ukiwa ni Beitul-Muqaddas

Serikali ya Syria kwa mara nyingine tena imesisiitiza kuwa, inaunga mkono kuundwa nchi huru ya Palestina mji wake mkuu ukiwa ni Beitul-Muqaddas.

Sisitizo hilo limetolewa na Faisal Miqdad, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Syria katika ujumbe wake kwa masaba wa tarehe 29 Novemba ambayo ni Siku ya Kimataifa ya Kuonesha Mshikamano na Taifa la Palestina iliyoadhimishwa jana na kubainisha kwamba, wananchi wa Palestina wana haki yan kujiainisha hatima na mustakabali wao.

Faisal Miqdad ameeleza bayana kwamba, Syria mbali na kuunga mkono kuundwa nchi huru ya Palestina inasisitiza kwamba, Beitul-Muqaddas ni sehemu ya Palestina na ardhi hiyo katu haiwezi kutenganishwa na taifa hilo madhulumu.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Syria amesema kuwa, tarehe 29 Novemba ambayo ni Siku ya Kimataifa ya Kuonesha Mshikamano na Taifa la Palestina imebadilika na kuwa jukwaa la kimataifa kwa ajili ya kuhuisha katika fikra za walimwengu malengo matukufu ya taifa la Palestina.

Faisal Miqdad, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Syria

 

Faisal Miqdad ameashiria hatari zinazoendelea kuikabili kadhia ya Palestina na kueleza bayana kwamba, hadi leo jamii ya kimataifa haichukua hatua za maana kwa ajili ya kuhitimisha uvamizi wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel katika ardhi za Wapalestina.

Aidha amesema, mataifa yanayouunga mkono utawala ghasibu wa Israel yanabeba dhima ya matokeo ya kuendelea jinai za utawala huo dhidi ya wanachi wasio na hatia wa Palestina na  kutaka Umoja wa Mataifa utekeleze majukumu yake iipasavyo mkabala wa maafa yanayowakabili wananchi hao.