Dec 02, 2021 03:00 UTC
  • HAMAS: Mabunge ya Kiarabu na Kiislamu yazuie kuanzishwa uhusiano wa kawaida na Israel

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imeyataka mabunge ya mataifa ya Kiarabu na Kiislamu yasimame kidete na kuzizuia serikali zao kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel.

Khalil al-Hayya, Mkuu wa Ofisi ya Mahusiano ya Kiarabu na Kiislamu ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS)  amesema hayo katika mkutano wa wawakilishi wa Mabunge Kwa Ajili ya Quds uliofanyikak nchini Uturuki na kuongeza kuwa, Mabunge ya Kiarabu na Kiislamu yanapaswa kuzuia mwenendo wa kuanzishwa uhusiano wa kawaida na Israel kwa kutunga na kuweka sheria ambayo itaitambua hatua ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala ghasibu wa Israel kuwa, ni kosa na uhalifu.

Afisa huyo mwandamizi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS)  amesema kuwa, hatua ya Uingereza ya kuiweka harakati hiyo katika orodha yake ya eti makundi ya kigaidi, haiilengi Hamas peke yake, bali wananchi wote wa Palestina.

Khalil al-Hayya, Mkuu wa Ofisi ya Mahusiano ya Kiarabu na Kiislamu ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina

 

Khalil al-Hayya amekosoa vikali hatua ya baadhi ya mataifa ya Kiarabu ya kuwasiliti wananchi madhulumu wa Palestina na kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala dhalimu wa Israel unaotenda jinai kila uchao dhidi ya Wapalestina.

Itakumbukwa kuwa, Septemba mwaka jana (2020), Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Imarati na Bahrain walisaini mkataba wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel katika hafla iliyofanyika katika Ikulu ya White House mjini Washington.

Baada ya hapo Sudan na Morocco nazo zikafuata mkumbo huo huo na kutangaza  kuanzisha uhusiano na utawala huo haramu, uamuzi ambao umeendelea kulalamikiwa na kulaaniwa na wapenda haki kote ulimwenguni.

Tags