Dec 02, 2021 07:08 UTC
  • Saudia yataka kuzuia uchunguzi wa ukiukaji haki za binadamu Yemen usifanyike

Gazeti la The Guardian la Uingereza limeripoti kuwa, Saudi Arabia inajaribu kuuzuia Umoja wa Mataifa usifanye uchunguzi wa ukiukaji haki za binadamu uliofanywa nchini Yemen.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, Saudia inaendelea kutoa mashinikizo kwa maafisa wa UN ili wasimamishe uchunguzi kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Yemen.

Ripoti ya Guardian inaonyesha kuwa, utawala wa Riyadh unatumia njia na mbinu tofauti ili kuzuia kufanyika uchunguzi wa aina yoyote kuhusiana na ukiukaji wa haki za binadamu uliofanywa Yemen.

Mwezi Oktoba mwaka huu pia, Saudi Arabia ilitoa mashinikizo kwa baadhi ya wanachama wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa ili kuzuia kurefushwa muda wa kazi ya tume huru ya uchunguzi wa jinai za kivita zilizofanywa na nchi hiyo huko Yemen.

Mfalme Salman bin Abdulaziz wa Saudi Arabia

Kwa msaada na uungaji mkono wa Marekani, Imarati na nchi zingine kadhaa, mwezi Machi 2015, Saudia ilianzisha uvamizi wa kijeshi dhidi ya Yemen ulioandamana na mzingiro wa nchi kavu, majini na angani ilioiwekea nchi hiyo masikini ya Kiarabu.

Moto wa vita uliowashwa na Saudi Arabia na waitifaki wake umeua na kujeruhi mamia ya maelfu ya Wayemen na kuwafanya wengine milioni nne kuwa wakimbizi.

Hujuma na mashambulio yaliyofanywa na Saudi Arabia na waitifaki wake vilevile yamebomoa na kuteketeza zaidi ya asilimia 85 ya miundomsingi ya Yemen na kuifanya nchi hiyo ikabiliwe na uhaba mkubwa wa chakula na dawa. 

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, Yemen inakabiliwa na hali mbaya zaidi ya maafa ya kibinadamu duniani.../