Dec 03, 2021 10:49 UTC
  • Iran na Syria kuimarisha zaidi ushirikiano wao wa kiuchumi na kibiashara

Waziri wa Uchumi wa Syria amesema kuwa, nchi yake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zina nia ya kweli ya kuimarisha zaidi na zaidi ushirikiano wao wa kiuchumi na kibiashara.

Shirika la habari la IRIB limeripoti hayo leo Ijumaa na kumnukuu Waziri wa Uchumi wa Syria, Samir al Khalil akisema wakati alipotembelea maonyesho maalumu ya bidhaa za Iran mjini Damascus, Syria kwamba, lengo letu si kuweko mabadilishao ya kibiashara tu baina ya Tehran na Damascus, bali tunachotaka ni kufaidika na uzoefu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kupambana na kufelisha vikwazo vya kidhulma vya madola ya Magharibi.

Waziri wa Uchumi wa Syria amegusia pia lengo la nchi yake la kutumia tajiriba na uzoefu wa Iran katika kuvifanya viwanda vya ndani ya nchi kutegemea kikamilifu teknolojia ya ndani bila ya kuwa na haja na wageni na kusema kuwa, hivi sasa kuna matatizo kadhaa katika juhudi za kuongeza kiwango na thamani ya mabadilishano ya biashara na Syria ikiwa ni pamoja na matatizo ya kusafirisha fedha, uchukuzi na sheria forodha.

Waziri wa Uchumi wa Syria, Samir al Khalil

 

Naye Masan Nahas, Naibu wa Ofisi ya Kibiashara ya Syria amesema wakati alipotembelea maonyesho hayo yanayoshirikisha mashirika 164 ya Iran, kuwa, kufanyika maonyesho maalumu ya bidhaa za Iran nchini Syria ni fursa nzuri sana ya kustawishwa zaidi na zaidi ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara baina ya nchi mbili.

Amesema, hivi sasa Iran na Syria zinapambana na vikwazo vya kidhulma vya madola ya Magharibi hivyo ni jambo la dharura kuweko ushirikiano wa moja kwa moja baina ya sekta za kiuchumi, wafanyabiashara na kila anayejishughulisha na masuala ya kiuchumi na kibiashara katika nchi hizo mbili.

Tags