Dec 04, 2021 04:42 UTC
  • Waziri wa Lebanon aliyekosoa hujuma ya Saudia Yemen ajiuzulu

Waziri wa Habari wa Lebanon George Kordahi amejiuzulu ili kupunguza mgogoro wa nchi yake na Saudi Arabia baada ya kauli yake ya kukosoa vita vya Saudia dhidi ya Yemen.

Kordahi ametangaza kujiuzulu kama waziri Ijumaa katika kikao na waandishi habari ambapo amesema ameamua kujiuzuli kwa sababu ameweka maslahi ya kitaifa ya Lebanon mbele ya mitazamo yake binafsi.

Amesema hakubali kuwa kisingizio cha kuwaharibia maisha Walebanon wanaoishi katika nchi za Kiarabu katika Ghuba ya Uajemi. Amesema katika siku za hivi karibuni kumeshuhudiwa kampeni ya makusudi katika baadhi  ya vyombo vya habari vya Lebanon na katika Ghuba ya Uajemi ambapo kumeongezeka mashinikizo ya kutaka ajiuzulu sambamba na mashinikizo makubwa yasiyo na uadilifu dhidi ya Lebanon.

Kordahi amesema Waziri Mkuu wa Lebanon Najib Mikati alimfahamisha mapema wiki hii kuwa, kujiuzulu kwake ni sharti ambalo limewekwa na Rais Emmanuel Macron kabla hajaanza jitihada za kupatanisha Saudia na Lebanon.

Watoto ni waathirika wakubwa wa vita vya Saudia dhidi ya Yemen

Kabla hajateuliwa waziri, Kordahi aliwahi kuikosoa vikali Saudi Arabia kwa kuanzisha vita dhidi ya Yemen na kusema vita hivyo ambavyo vimedumu zaidi ya miaka saba haviwezi kuendelea milele. Katika mahojiano ya Mwezi Agosti ambayo yalirushwa hewani Oktoba baada ya kuteuliwa waziri, Kordahi alisema vita dhidi ya Yemen ni uvamizi ambao unatekelezwa na Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu. Alisema vita hivyo ni vya kipuuzi na vinapaswa kusitishwa huku akisema anapinga vita baina ya mataifa ya Kiarabu. Kordahi aidha alisema askari wa  Jeshi la Yemen na wapiganaji wa Kamati za Kujitolea za Wananchi wanajitetea mbele ya uvamizi wa kigeni kwani muungano wa kivita wa Saudia hushambulia makazi ya raia, vijiji, maziko na harusi.

Matamshi ya Kordahi yaliikera sana Saudia ambayo ilivunja uhusiano wake na Lebanon na hatua hiyo ikafuatwa na UAE, Bahrain na Kuwait.

Tags