Dec 04, 2021 07:35 UTC
  • Ndege za kivita za Saudia zaua raia 16 Yemen

Ndege za kivita za muungano vamizi wa Saudia zimedondosha mabomu katika wilaya ya Maqbanah mkoani Taiz nchini Yemen na kuua raia wasiopungua 16.

Kwa mujibu wa ripoti ya Ijumaa usiku ya Televisheni ya Al Masirah, watoto ni miongoni mwa walipoteza maisha katika shambulizi hilo la ndege za kivita za Saudia.

Hali kadhalika ndege za kivita za Saudia Ijumaa usiku zimedondosha mabomu mara mbili katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Sanaa na maeneo ya karibu.

Muungano vamizi wa Saudia umekithirisha mashambulizi dhidi ya maeneo ya raia katika mikoa kadhaa ya Yemen. 

Kufuatia uungaji mkono wa Marekani, Imarati, utawala haramu wa Israel na nchi nyingine kadhaa za Kiarabu, Saudi Arabia iliivamia kijeshi nchi masikini ya Yemen mnamo Machi 2015 na kuiwekea mzingiro wa pande zote wa nchi kavu, anga na majini. Uvamizi wa kijeshi wa Saudia umeisababishia pia nchi masikini ya Yemen uhaba mkubwa wa chakula na dawa.

Watoto ni waathirika wakuu wa hujuma za Saudia dhidi ya Yemen

Hivi karibuni  Shirika la Entesaf la Kupigania Haki za Wanawake na Watoto lenye makao yake nchini Yemen, limesema watoto zaidi ya 300 wa Kiyemen wanaaga dunia kila siku kutokana na utapiamlo wa kiwango cha juu, hali ambayo imesababishwa na vita vya Saudia dhidi ya nchi hiyo.

Hadi hivi sasa uvamizi huo wa Saudia na waitifaki wake umeshasababisha makumi ya maelfu ya Wayemen kuuawa, wengine wengi kujeruhiwa huku mamilioni ya wengine wakiwa wakimbizi ndani na nje ya nchi.