Dec 04, 2021 11:25 UTC
  • Hania: Mwenendo wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel unapaswa kusitishwa mara moja

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) amesema kuwa, Umma wa Kiislamu unapaswa kufanya juhudi za kusitisha sera za kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel.

Ismail Hania amesema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na Shirika la Habari la Mehr na kusisitiza kwamba, kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala ghasibu wa Israel ni jambo ambalo linapasa kusitishwa haraka iwezekanavyo, kwani sera kama hizi hazina kitu kingine ghairi ya shari na ubaya.

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema, kuanzisha uhusiano wa kawaida na Wazayuni ni jambo linalopelekea kuibuka maswali kuhusiana na haiba ya Umma wa Kiislamu na linaangamiza historia yake.

Aidha Ismail Hania amesema kuwa, "tunautaka Umma wote wa Kiislamu uingie uwanjani na kufanya juhudi za kusitisha mwenendo huu wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na maghasibu Wazayuni. 

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) ameyataka mataifa ya Kiarabu ambayo yameanzisha uhusiano wa kawaida na utawala dhalimu wa Israel kuangalia upya siasa zao.

Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Imarati na Bahrain baada ya kutia saini hati ya kuanzisha uhusiano na Israel

 

Itakumbukwa kuwa, Septemba mwaka jana (2020), Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Imarati na Bahrain walisaini mkataba wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel katika hafla iliyofanyika katika Ikulu ya White House mjini Washington.

Baada ya hapo Sudan na Morocco nazo zikafuata mkumbo huo huo na kutangaza  kuanzisha uhusiano na utawala huo haramu, uamuzi ambao umeendelea kulalamikiwa na kulaaniwa na wapenda haki kote ulimwenguni.