Dec 05, 2021 02:37 UTC
  • Marekani yaendelea kushirikiana na Saudi Arabia katika vita vya Yemen

Mashambulio ya mabomu dhidi ya Yemen yanayofanywa na jeshi la muungano unaoongozwa na Saudi Arabia yanaendelea huku nchi za Magharibi, zinazotoa nara za kutetea haki za binadamu hususan Marekani, zikiendelea kuisaidia Saudi Arabia katika kutenda jinai dhidi ya wananchi wa Yemen.

Kuhusiana na suala hilo, seneta Bernie Sanders na Ro Khanna ambaye ni mjumbe wa Baraza la Wawakilishi la Marekani, wamekiri katika taarifa yao kwamba Saudi Arabia inaendelea kuishambulia Yemen kwa mabomu kwa msaada wa Marekani. Wabunge hao wawili wa Kongresi ya Marekani wameitaka serikali ya Washington kuishinikiza Saudi Arabia ikomeshe vita vya Yemen na kuondoa mzingiro wa nchi hiyo wakisema uvamizi na vita vya wa Saudia huko Yemen vimesababisha maafa makubwa zaidi ya kibinadamu duniani.

Vita vya Saudi Arabia dhidi ya Yemen vilivyoanza mwaka 2015 vinaendelea na tayari vimeua na kujeruhi mamia kwa maelfu ya Wayemeni wasio na hatia na kuwalazimisha wengine zaidi ya milioni 4 kuyahama makaazi yao. Uvamizi huo wa kijeshi wa Saudia pia umeharibu zaidi ya asilimia 85 ya miundombinu ya Yemen na kuifanya nchi hiyo isumbuliwe na uhaba mkubwa wa chakula na dawa. Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya kibinadamu, Martin Griffiths, ameitaja hali ya kibinadamu nchini Yemen kuwa maafa na kusema: "Yemen inapitia mzozo mbaya zaidi wa binadamu duniani."

Yemen

Saudi Arabia na washirika wake wanaendelea kuishambulia Yemen kwa uungaji mkono na misaada ya Marekani na nchi za Magharibi. Hii ni licha ya kwamba, hivi karibuni serikali ya Joe Biden iliahidi kumaliza vita nchini Yemen na kudai kwamba imezuia uuzaji wa silaha za mashambulio kwa Wasaudi. Hata hivyo na licha ya ahadi zote hizo, uungaji mkono na misaada ya Marekani kwa Saudi Arabia inaendelea kupitia njia ya mauzo ya silaha na kuendeleza uhusiano wa kisiasa na kiuchumi na utawala wa Riyadh unaoua watoto na wanawake wa Yemen. Gazeti la The Guardian limeandika: "Kinyume na madai yake ya kukomesha operesheni na mashambulizi ya kijeshi huko Yemen, serikali ya Biden haijafanya hivyo, na mgogoro wa nchi hiyo bado unaendelea."

Hivi sasa wanakandarasi wa ulinzi wa Marekani wanaendelea kutoa huduma kwa ndege za Saudi zinazoshiriki katika vita dhidi ya watu wa Yemen. Hivi karibuni pia Marekani ilitangaza kuuza silaha mpya kwa Wasaudia. Takwimu zilizochapishwa zinaonyesha kuwa, thamani ya mikataba ya silaha iliyotiwa saini kati ya Marekani na Saudi Arabia tangu Machi 2015 inakaribia dola bilioni 28.5, na katika kipindi cha utawala wa Joe Biden pekee mikataba 20 yenye thamani ya dola bilioni 1.2 imetiwa saini baina ya nchi hizo mbili. Nukta ya kuvutia ni kwamba, licha ya uungaji mkono wote huo wa Marekani kwa Riyadh, vikosi vya muungano vamizi wa Saudia vinaendelea kupata kipigo na hasara kubwa katika vita vya Yemen. Abdul Wahab al-Mahbashi, mjumbe wa Idara ya Siasa ya Ansarullah anasema: "Marekani inahisi kuwa imepoteza karata zake zote za turufu katika kanda ya Magharibi mwa Asia, hasa zile zinazohusiana na vita vya Yemen."

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yakiwemo Shirika la Afya Duniani na UNICEF yamekuwa yakionya mara kwa mara kwamba watu wa Yemen wanakabiliwa na njaa na maafa ya binadamu kutokana na kuendelea mashambulizi ya muungano vamizi unaoongozwa na Saudia. Yemen pia inasumbuliwa na hali mbaya ya uchumi baada ya kuwa katika vita vya kujihami vya miaka kadhaa sasa. Maeneo mengi ya Yemen wanasumbuliwa na umaskini na magonjwa, na janga la corona na mahitaji ya dawa na matibabu ni tatizo kubwa kwa raia wengi wa nchi hiyo. Ripoti za kimataifa zinaonesha kuwa, mamilioni ya watu katika nchi hiyo wako kwenye ncha ya kutumbukia kwenye baa la njaa. 

Watoto wa Yemen

Katika hali hiyo, wajumbe wawili wa Kongresi ya Marekani wamepinga siasa za Biden za kuendelea kuiunga mkono Saudi Arabia katika vita vya Yemen; japokuwa inaonekana kwamba tahadhari hiyo kama zilivyokuwa za kabla yake, itapuuzwa na viongozi wa sasa wa White House. 

Tags