Dec 05, 2021 11:03 UTC
  • Onyo kuhusu hatari ya kupata nguvu tena genge la Daesh eneo la Kurdistan nchini Iraq

Mkuu wa chama cha Democrat cha eneo la Kurdistan la Iraq na ambaye pia ni rais wa serikali ya ndani ya eneo hilo ameonya kuhusu hatari ya kupata nguvu upya genge la Daesh (ISIS) kwenye eneo hilo.

Katika kipindi cha wiki moja iliyopita, eneo la Kurdistan la Iraq limekumbwa na mashambulio mawili ya kigaidi yaliyofanywa na mabaki ya magaidi wa Daesh au ISIS. Wizara ya Peshmerga ya Kurdistan ya Iraq ilitangaza siku ya Jumapili ya tarehe 28 Novemba kwamba askari watano wa Peshmerga waliuawa katika shambulio lililohusishwa na genge la kigaidi la Daesh katika eneo la Garmiyan. Kwa mujibu wa tangazo hilo, gari lililokuwa limewabeba askari wa Peshmerga lilikanyaga bomu na kuripuka katika eneo hilo. Askari wanne wa Peshmerga walijeruhiwa katika shambulio hilo. Siku ya Alkhamisi ya tarehe pili Disemba pia, magaidi wa Daesh walivamia kijiji kimoja cha Wakurdi katika eneo lenye utawala wa ndani la Kurdistan la Iraq  na kuua wanavijiji watatu kabla ya kukimbia.

Mashambulizi ya mabaki hayo ya genge la ukufurishaji la Daesh yamezusha hofu na wasiwasi kwa wakuu wa Kurdistan ya Iraq. Nechirvan Barzani, rais wa mamlaka ya ndani ya Kurdistan ya Iraq amesema kuwa, mashambulio hayo ni kengele ya hatari sana kwa eneo hilo. Naye Masrour Barzani, waziri mkuu wa serikali ya ndani ya Kurdistan ya Iraq amesema, genge la ISIS ni tishio kwa usalama wa wakazi wa eneo hilo. Siku ya Jumanne, Masoud Barzani, mkuu wa chama cha Democrat cha Kurdistan ya Iraq alitahadharisha kuwa, hatari kubwa inalijongelea eneo hilo kutoka kwa genge la kigaidi la Daesh.

Wapiganaji wa Peshmerga wa Kurdistan ya Iraq

 

Mashambulizi ya genge la ukufurishaji la ISIS katika eneo la Kurdistan nchini Iraq yamefanyika katika hali ambayo katika siku za hivi karibuni eneo hilo limekumbwa na maandamano ya wananchi hasa ya wanafunzi wa vyuo vikuu wanaolalamikia utendaji mbovu wa serikali ya ndani ya eneo hilo. Kwa ufupi ni kwamba usalama wa kijamii katika eneo la Kurdistan huko Iraq umekumbwa na changamoto nzito katika siku za hivi karibuni.

Mbali na hayo, mashambulizi ya genge la Daesh katika eneo hilo yamefanyika katika mazingira ambayo, umebakia muda wa chini ya mwezi mmoja tu hadi kufika wakati ambao wanajeshi wa Marekani wanapaswa kuondoka nchini Iraq. Kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa baina ya Waziri Mkuu wa Iraq, Mustafa al Kadhimi na rais wa Marekani, Joe Biden, wanajeshi wa Marekani wanapaswa wawe wameondoka nchini Iraq ifikapo mwishoni mwa mwezi huu wa Disemba. Baadhi ya wakuu wa eneo la Kurdistan la Iraq ni miongoni mwa wanaopinga kuondoka wanajeshi wa Marekani nchini humo.

Kiujumla ni kwamba kila linaposhika kasi suala la kuondoka wanajeshi wa Marekani nchini Iraq, genge la kigaidi la ISIS hujitokeza na kuzidisha mashambulio yake ya kigaidi ili kuwapa Wamarekani kisingizio cha kuendelea kubakia nchini humo. Hivyo si jambo lililo mbali kuamini kwamba mashambulio ya kigaidi ya wiki moja iliyopita yaliyofanywa na mabaki ya magaidi wa Daesh katika baadhi ya maeneo ya Kurdistan nchini Iraq, ni mpango maalumu uliofanywa na magaidi hao kwa uratibu na baraka za Wamarekani ili kuwapa kisingizio cha kutoondoka huko Iraq.

Wanajeshi vamizi wa Marekani nchini Iraq

 

Tukumbuke kuwa, mwaka 2014 wakati magaidi wa Daesh walipokaribia kabisa kuliteka eneo ha Kurdistan la Iraq, Wamarekani hawakuwa tayari kuisaidia serikali ya ndani ya eneo hilo. Nchi pekee iliyokwenda na kuliokoa eneo la Kurdistan nchini Iraq, ilikuwa ni Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Serikali ya ndani ya eneo la Kurdistan nchini Iraq ina deni kubwa kwa Luteni Jenerali shahid Qassem Soleimani, Kamanda wa zamani wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH kwa kuliokoa eneo hilo na serikali yake iliyokuwa imekaribia mno kusambaratishwa na magaidi wa Daesh.

Nukta nyingine ya kuiashiria hapa ni kwamba, mashambulio ya magaidi wa ISIS yamefanyika huko Kurdistan Iraq katika hali ambayo, bado kuna mivutano baina ya askari wa Peshmerga na jeshi la serikali kuu ya Iraq. Rais wa serikali ya ndani ya Iraq amesema kuwa, vitisho vya kiusalama vinavyotokana na mashambulio ya genge la kigaidi la ISIS vinawajibisha kuchukuliwa hatua za haraka za kuondolwa mizozo baina ya jeshi la serikali kuu na maeneo ambayo usalama wake unasimamiwa na askari wa Peshmerga.

Tags