Dec 05, 2021 14:26 UTC
  • Saudia yaendelea kumwaga damu za raia nchini Yemen

Kwa akali watu 30 wameuawa na kujeruhiwa kufuatia mashambulio ya anga ya muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na utawala wa Aal-Saud dhidi ya mji mkuu wa Yemen, Sana'a.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Iran Press, watu 16 wameuawa huku wengine wasiopungua 16 wakijeruhiwa katika hujuma za anga za ndege za kivita za muungano huo vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya makazi ya raia jijini Sana'a usiku wa kuamkia leo.

Habari zaidi zinasema kuwa, mashambulio hayo ya anga mbali na kuuwa na kujeruhi, lakini pia yameharibu kikamilifu majengo yenye makazi ya raia wa Yemen wasio na hatia, pamoja na duka la mboga mjini Sana'a.

Juzi Ijumaa pia, ndege za kivita za muungano vamizi wa Saudi Arabia zilidondosha mabomu katika wilaya ya Maqbanah mkoani Taizz na kuua raia wasiopungua 30 na makumi ya wengine kujeruhiwa.

Uharibifu uliosababishwa na hujuma za anga za Saudia nchini Yemen

Ofisi ya Haki za Binadamu katika mkoa wa Taizz nchini Yemen imelaani vikali jinai za utawala vamizi wa Saudi Arabia na washirika wake dhidi ya wananchi wa Yemen.

Wakati huo huo, Muhammad Abdulsalam, Msemaji wa Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen amelaani jinai zinazoendelea kufanywa na muungano vamizi wa Saudia dhidi ya raia wasio na hatia wala ulinzi wa nchi yake.