Dec 27, 2021 02:44 UTC
  • Jumuiya za kutetea haki za binadamu: Saudia imekamata dazeni ya wanaharakati wa kike mwaka 2021

Shirika la kutetea haki za binadamu limetoa tahadhari kuhusu hali mbaya ya haki za binadamu nchini Saudi Arabia, likisema dazeni ya wanaharakati mashuhuri wa haki za wanawake wamekamatwa kiholela na askari wa utawala wa Riyadh katika kipindi chote cha mwaka huu.

Shirika la kutetea haki za binadamu la Sanad ambalo linafuatilia na kufichua ukiukaji wa haki za binadamu nchini Saudi Arabia, limetangaza kwamba wanaharakati hao waliwekwa kizuizini katika miji mbalimbali ya utawala wa kifalme wa nchi hiyo, kama sehemu ya ukandamizaji na ukatili unaoongozwa na Mwanamfalme Mohammed bin Salman dhidi ya wanaharakakti na wapinzani wa kisiasa.

Shirika hilo la Sanad limesema kuwa, zaidi ya wanaharakati 100 wa kike wamekamatwa tangu mwanamfalme huyo mwenye umri wa miaka 36 ateuliwe kuwa mrithi wa ufalme wa Saudi Arabia miaka minne iliyopita, na kwamba 60 kati yao wangali wanateseka gerezani.

Shirika hilo la kutetea haki za binadamu limesisitiza kuwa, utawala wa Saudi Arabia unapaswa kuwajibishwa kikamilifu kwa ukiukaji wa haki za kijamii na haki ya uhuru wa maoni na kujieleza.

Mapema mwezi huu, zaidi ya wabunge 120 wa Bunge la Ulaya walilaani "mateso na manyanyaso yanayoendelea kufanywa na utawala Saudi Arabia dhidi ya watetezi wa haki za wanawake wakisema hata wanaharakati walioachiliwa huru bado wanakabiliwa na vikwazo vikali na ukiukwaji wa haki zao. 

Katika barua ya pamoja iliyotiwa saini kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Watetezi wa Haki za Kibinadamu, wabunge hao walisisitiza wito wao kwa utawala wa Saudia "kuwaachilia mara moja na bila masharti wanawake wote wanaolengwa kutokana na harakati zao za kutetea haki za binadamu."

Tangu Bin Salman alipoteuliwa kuwa mrithi wa ufalme wa Saudi Arabia mwaka wa 2017, utawala wa nchi hiyo umeongeza kasi ya kukamatwa wanaharakati, wanablogu, wasomi na wapinzani wa kisiasa wa utawala huuo.

Shekh Baqir Nimr alinyongwa na utawala wa kifalme wa Saudia

Wanazuoni wa Kiislamu wamenyongwa, na watetezi wa haki za wanawake wamewekwa korokoroni na kuteswa, huku uhuru wa kujieleza, kujumuika na imani ukiendelea kubinywa na kukandamizwa.

Tags