Dec 31, 2021 12:32 UTC
  • Iraq na tatizo sugu la ugaidi

Japokuwa mtandao wa kigaidi wa DAESH (ISIS) umetokomezwa nchini Iraq, lakini kutokana na sababu tofauti, kitisho cha ugaidi kingali kipo nchini humo.

Katika siku za karibuni, zilitangazwa habari tatu kuhusu tatizo hilo sugu la ugaidi nchini Iraq. Habari ya kwanza ni kwamba, kundi la kigaidi la Daesh limemteka nyara Yasir al Jawrani, afisa wa wizara ya mambo ya ndani, ambaye pia ni mkurugenzi wa Idara ya Pasi za Kusafiria ya Al Aadhamiyyah pamoja na marafiki zake watatu katika kitongoji cha Khaaniqin kilichoko mkoani Diyala, kisha likawaua shahidi kikatili na kinyama Wairaqi hao wanne kwa kuwakata vichwa.

Yasir al Jawrani

Habari ya pili ni kwamba, Sabah an-Nuuman, msemaji wa shirika la kupambana na ugaidi la Iraq amesema, katika mwaka huu uliomalizika wa 2021, kikosi cha kupambana na ugaidi cha shirika hilo kimetekeleza operesheni zaidi ya 300; na katika operesheni hizo, mbali na kutokomezwa maficho ya Daesh, magaidi 100 wa genge hilo la ukufurishaji waliangamizwa na zaidi ya wengine 250 walikamatwa.

Na habari ya tatu ni kuwa, watu wawili waliokuwa na silaha, walitaka kumuua afisa mmoja wa shirika la intelijensia na la kupambana na ugaidi la Addiwaniyah katika eneo la Hayyu-shurtah. Afisa huyo alijeruhiwa katika shambulio hilo la kigaidi na akakimbizwa na kupelekwa hospitali ya Addiwaniyah kwa ajili ya kutibiwa.

Tatizo sugu la ugaidi halikuanza leo nchini Iraq, bali chimbuko lake lilianzia tangu miongo miwili nyuma. Kwa hakika ugaidi ni matokeo ya siasa za Marekani kuhusiana na Iraq. Kusambaratisha miundomsingi ya kijeshi na kiusalama ya Iraq ni matunda ya siasa na sera zilizotekelezwa na Mareani katika nchi hiyo.

Askari wa jeshi la kigaidi la Marekani nchini Iraq

Baada ya kujitokeza ombwe la kiusalama na kijeshi, ndipo makundi ya kigaidi yalipopata fursa na uwanja wa kujitokeza na kujifaragua nchini Iraq. Kwa sababu ya manufaa na maslahi ya kisiasa na kiusalama ya Marekani na washirika wake katika eneo, baadhi ya makundi hayo yalikuwa hata yakisaidiwa na kuungwa mkono na nchi hizo; na ndio maana hata baada ya Daesh kuvamia na kuishambulia kijeshi Iraq, mapambano dhidi ya kundi hilo hayakupewa uzito na waungaji mkono wake hao, mpaka pale kundi hilo la kigaidi na ukufurishaji lilipogeuka kuwa tishio kwa Magharibi.

Nukta nyingine muhimu ni kwamba, wakati tishio la ugaidi kwa usalama na umoja wa ardhi yote ya Iraq lilipofikia kiwango cha juu kabisa, ilitolewa fatua na Kiongozi wa Juu wa kidini wa Iraq ya kuunda jeshi la kujitolea la wananchi la Al Hashdu-Sha'abi, ambalo ndilo lililotoa mchango muhimu na mkubwa zaidi katika kupambana na ugaidi wa Kidaesh.

Katika harakati za kupambana na ugaidi, makamanda wa Muqawama, akiwemo Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu yaani Sepah, na Abu Mahdi al Muhandis, Naibu Mkuu wa jeshi la kujitolea la wananchi wa Iraq la al Hashdu-Sha'abi, walitoa mchango mkubwa sana; lakini mnamo Januari 3, 2020, jeshi la kigaidi la Marekani liliwaua shahidi makamanda hao karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad ili kuudhoofisha muqawama wa Iraq katika vita dhidi ya ugaidi. Ukweli ni kwamba, hatua hiyo ya serikali ya Marekani ilikuwa sawa na kutoa huduma na msaada mkubwa kwa makundi ya kigaidi na hasa ugaidi wa Kidaesh nchini Iraq.

Shahidi Qassem Soleimani (kushoto) na Shahidi Abu Mahdi al Muhandis

Hivi sasa, na hata kama ugaidi hautishii tena umoja wa ardhi yote ya Iraq, lakini tatizo sugu la mauaji ya kigaidi lingali linaisokota nchi hiyo, ambapo kwa sasa, raia ndio wanaokabiliwa na tishio la hujuma za makundi ya kigaidi. Kama tulivyogusia hapo kabla, katika mwaka huu tu uliomalizika wa 2021, shirika la kupambana na ugaidi la Iraq lilitekeleza operesheni zaidi ya 300 dhidi ya ugaidi. Hii inaonyesha kuwa tatizo sugu la ugaidi lingalipo nchini Iraq na halijamalizika moja kwa moja.

Harakati za kigaidi nchini Iraq zimeshtadi katika hali ambayo, kuna mambo mawili yenye umuhimu maalumu kwa nchi hiyo kwa sasa. La kwanza ni kuhusu kuondoka wanajeshi wa Marekani. Baadhi wachambuzi wanaitakidi kuwa, kuongezeka harakati za magaidi kunafanyika kwa lengo la kulikuza dai la udharura wa kuendelea kuwepo wanajeshi wa Marekani nchini Iraq. Na jambo la pili ni kuhusu hali tete ya kisiasa na kiusalama iliyojitokeza nchini humo baada ya uchaguzi wa bunge uliofanyika Oktoba 10. Ukweli ni kwamba hivi sasa makundi na mirengo ya kisiasa  ya Iraq inatakiwa ichukue hatua za kufikia mwafaka wa pamoja na kuandaa mazingira ya kuundwa serikali mpya ili kupunguza joto la hali hiyo tete inayotawala nchini humo. Hali tete ambayo inayaandalia uwanja mzuri makundi ya kigaidi wa kuendesha harakati zao.../

Tags