Jan 02, 2022 15:23 UTC
  • Miaka sita tangu kunyongwa Sheikh Nimr, ukandamizaji unaongezeka Saudia

imepita miaka sita sasa tangu utawala wa kifalme wa Saudi Arabia ulipomnyonga manazuoni mashuhuri wa Kiislamu Sheikh Nimr Baqir al-Nimr, ambaye alitoa wito wa kuwepo demokrasia katika nchi hiyo na kuitisha maandamano dhidi ya utawala huo

Tangazo lililotolewa na utawala wa Saudia mnamo Januari 2, 2016 kwamba umemuua mwanazuoni huyo aliyekuwa na umri wa miaka 56 pamoja na wafungwa wengine 46 liliibua hasira kali na malalamiko makubwa katika nchi mbalimbali hususan katika mji aliozaliwa mashariki mwa Saudi Arabia, ambapo Waislamu wa madhehebu ya Shia wanalalamika kutokana na kutengwa, kubaguliwa na kunyanyaswa wka sababu ya imani yao.

Sheikh Nimr Bari al Nimr, mwanazuoni maarufu wa Saudia alikamatwa na utawala wa ukoo wa Aal Saudi manamo Julai 2012 na hatimaye Oktoba 2015, mahakama ya utawala wa Saudia ilimhukumu msomi huyo wa Kiislamu kifo cha kukatwa kichwa kwa panga na kusulubiwa kadamnasi kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kula njama dhidi ya utawala wa nchi hiyo..

Hukumu hiyo ilitekelezwa tarehe Pili Januari mwaka 2016. Kuuawa kwa msomi na mwanaharakati huyo kulipingwa vikali na jumuiya za kikanda na kimataifa za kutetea haki za binadamu.   

Kesi ya Sheikh Nimr ilifanyika bila ya kuhudhuriwa na watu na alinyimwa haki ya kuwa na wanasheria. Utawala wa Saudia ulikataa kukabidhi mwili wa mwanazuon huyo wa Kiislamu kwa familia yake na kumzika kwenye kaburi lisilojulikana.

Msomii huyo wa Kiislamu alikuwa kinara wa maandamano yaliyotokea mwaka 2011 katika eneo la mashariki mwa Saudi Arabia la Qatif lenye Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Saudi Arabia, ambalo pia lina hifadhi kubwa zaidi ya mafuta ya nch hiyo japo wakazi wake wanaishi katika hali isiyoridhia kiuchumi.

Sheikh Baqir al Nimr hakuwahi kukanusha mashtaka ya kisiasa dhidi yake, lakini alisisitiza kuwa hajawahi kubeba silaha au kuchochea vurugu.

Sheikh Baqir al Nimr aliheshimiwa kama kiongozi na shujaa wa wakazi wa eneo hilo la Saudia kutokana na upinzani wake wa mara kwa mara dhidi ya kutengwa, dhuluma na ukandamizaji katika Jimbo la Mashariki lenye Waislamu wa madhebu ya Shia, na kudai mageuzi ya kisiasa, uhuru wa kujieleza na kuachiliwa huru wafungwa wa kisiasa. Vilevile alitoa wito wa kukomeshwa ubaguzi wa kiuchumi, kidini na kisiasa katika nchi ya Saudi Arabia. 

Tags