Jan 04, 2022 07:56 UTC
  • Nasrullah: Kupuuza uwepo wa US nchini Iraq, ni sawa na kumuua tena shahidi Soleimani

Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema kitendo cha kupuuza uwepo wa vikosi vamizi vya Marekani nchini Iraq, ni sawa na kuuawa shahidi kwa mara ya pili Luteni Jenerali Qasem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Sayyid Hassan Nasrulllah ameyasema hayo katika hotuba aliyoitoa jana usiku kwa mnasaba wa kuwadia mwaka wa pili tangu alipouawa shahidi Kamanda Soleimani na kuongeza kuwa, Marekani iliikalia kwa mabavu Iraq na kutekeleza mauaji ya halaiki, hata kabla ya kumuua shahidi Haji Qasem Soleimani.

Sayyid Nasrullah amebainisha kuwa, Marekani ililiasisi kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) kwa shabaha ya kurejesha silaha zake nchini Iraq, na kwa msingi huo inapaswa kubebeshwa dhima ya jinai zote zilizofanywa na genge hilo la kigaidi.

Amesema kinyume na Marekani ambayo inatekeleza jinai na mauaji ya kutisha kila uchao nchini Iraq, Jenerali Soleimani alisimama bega kwa bega na wananchi wa Iraq na kuwasaidia kuunda na kuimarisha mrengo wa muqawama.

Kamanda Soleimani

Sayyid Nasrullah amekumbusha kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ndilo lilikuwa taifa la kwanza kuliunga mkono taifa la Iraq katika vita dhidi ya genge la ISIS lililoundwa na Marekani. Amesema haingii akilini kuwafananisha mashahidi waliouawa wakiiunga mkono Iraq, na Wamarekani wanaotenda jinai na mauaji dhidi ya Wairaqi.

Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon ameeleza bayana kuwa, Shahidi Soleimani alikuwa na mchango mkubwa wa kuundwa kambi ya muqawama katika nchi za Iraq na Syria mkabala wa vikosi vamizi vya Marekani.

Tags