Jan 13, 2022 11:41 UTC
  • Al-Wifaq: Wananchi wa Bahrain wataendelea kudai haki zao kwa njia ya amani

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Mwafaka wa Kiislamu na Kitaifa nchini Bahrain (Al Wifaq) amesema kuwa, wananchi wa nchi hiyo wataendelea kudai haki zao kwa njia ya amani na kwamba, katu hawatasalimu amri katika njia hiyo.

Sheikh Ali Salman, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Mwafaka wa Kiislamu na Kitaifa nchini Bahrain (Al Wifaq) ametoa ujumbe huo akiwa jela na kueleza kwamba, kwa mujibu wa sheria na kanuni za Umoja wa Mataifa anaendelea kushikiliwa kidhulma na kinyume kabisa na sheria.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Mwafaka wa Kiislamu na Kitaifa nchini Bahrain (Al Wifaq) amewashukuru wale wote wanaoonyesha kuwa pamoja naye na wanaotaka kuweko mageuzi, demokrasia, uhuru, heshima na kuheshimiwa haki za raia nchini Baharain hususan familia za mashahidi na majeruhi na kubainisha kwamba, wananchi wa nchi hiyo wana haki ya kuwa na haki ndogo na za awali kabisa.

Maandamano ya kutaka kuachiliwa huru wafungwa nchini Bahrain

 

Jumuiya ya Mwafaka wa Kiislamu na Kitaifa nchini Bahrain (Al Wifaq) imekuwa ikitangaza kuwa, hatua ya utawala wa kifamilia wa Aal-Khalifa za kufanya ukandamizaji na mbinu nyingine zisizo za kisheria zimeifanya nchi hiyo kugeuka na kuwa jela kubwa ambayo ndani yake hakuna mtu mwenye haki ya kusema hata neno moja.

Nchi ya Bahrain ni kisiwa kidogo kilichoko katika Ghuba ya Uajemi ambapo utawala wa kifamilia wa Aal Khalifa ndiyo unaotawala nchini humo. 

Wananchi wa Bahrain wamekuwa wakifanya maandamano dhidi ya utawala wa Aal Khalifa kuanzia mwaka 2011 hadi sasa wakitaka kufanyika marekebisho makubwa nchini humo. 

Tags