Jan 14, 2022 03:10 UTC
  • Saudia yashambulia kwa mabomu hospitali Yemen, kadhaa wauawa

Ndege za kivita za muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia zimedondosha mabomu katika majengo ya makazi ya watu na hospitali katika mikoa ya Yemen ya Sana'a na Hudaydah, na kuua raia kadhaa.

Kanali ya televisheni ya al-Masirah iliripoti hayo jana Alkhamisi na kuelekeza kuwa, raia wawili wameuawa, huku wahudumu wanne wa hospitali moja katika kijiji cha Al-Sawad, wilaya ya Sanhan mkoani Sana'a wakijeruhiwa vibaya kufuatia hujuma hiyo ya anga.

Inaelekezwa kuwa, wawili miongoni mwa wahudumu hao wa afya wapo katika hali mahututi kutokana na majeraha mabaya waliyoyapata kufuatia shambulizi hilo la mabomu, kusini mwa mji mkuu wa Yemen, Sana'a.

Kwa mujibu wa al-Masira, kwa akali raia wawili wengine wameuawa kufuatia hujuma zingine za anga zilizofanywa na ndege za kijeshi za muungano vamizi katika wilaya ya al-Garrahi, mkoani Hudaydah.

Hospitali iliyoshambuliwa Yemen

Saudi Arabia huku ikiungwa mkono na Marekani, Imarati na nchi nyingine kadhaa zilianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen Machi 2015 na kuiwekea nchi hiyo mzingiro wa baharini, anga, na nchi kavu.

Vita hivyo aidha hadi sasa vimeuwa makumi ya maelfu ya wananchi wa Yemen na kuwafanya mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi, mbali na kuharibu asilimia kubwa ya miudomsingi ya nchi hiyo maskini ya Kiarabu.